Rafiki yangu mpendwa, hizi ni tano za juma hili namba 35 tunalomaliza kwenye mwaka huu 2018.

#1 KITABU NILICHOSOMA; UNAKOSEA KWA JINSI UNAVYOFANYA KAZI.

Juma hili nilipata nafasi ya kusoma vitabu vitatu, na moja ya vitabu hivyo ni REWORK kilichoandikwa na waanzilishi wa kampuni ya BASECAMP, Jason Fried na David Hansson, inayojihusisha na kutoa huduma za mtandao wa intaneti.

Waandishi wameandika kitabu hichi cha REWORK kama ushuhuda wao kwa jinsi wamekuwa wanaendesha kampuni yao tangu mwaka 1999 bila ya kufuata kanuni za kibiashara zilizozoeleka. Kampuni yao imekuwa inakua mwaka hadi mwaka licha ya kufanya kinyume kabisa na namna kampuni na biashara zilivyozoea kuendeshwa.

Kila nilichosoma kwenye kitabu hiki kina nguvu sana, nimejikuta naandika kila kitu na hivyo ni moja ya vitabu vichache vya kurudia rudia kusoma ili mtu uweze kuelewa na kufanyia kazi yale ambayo waandishi wanatushirikisha, ukiwa ni ushuhuda wa jinsi wanavyoendesha biashara yao.

Karibu nikushirikishe yale muhimu niliyoondoka nayo kwenye kitabu hiki;

  1. Utakapochagua kuendesha biashara yako kwa namna ambayo ni sahihi kwako, wengi watakukosoa na kukupinga, huna haja ya kubishana nao, unachohitaji kuweka juhudi na matokeo ya tofauti unayoyapata ndiyo yatakayobishana nao.
  2. Usiogope kwenda kinyume na wengi, kama unachotaka kufanya unajua ni sahihi. Kufuata kundi ni njia rahisi sana ya kushindwa.
  3. Zama hizi kila mtu anaweza kuingia kwenye biashara, teknolojia imerahisisha sana uendeshaji wa biashara. Mtu mmoja anaweza kuendesha biashara ambayo zamani ingehitaji watu watatu ili kuendesha.
  4. Wengine kushindwa haimaanishi na wewe utashindwa. Kama wengine wamejaribu njia ya tofauti wakashindwa, haimaanishi wewe usijaribu kwa sababu utashindwa. Wao wameshindwa, kwa sababu zao wenyewe, wewe jaribu na weka juhudi, kushindwa kwao hakumaanishi na wewe umeshindwa, tena kabla hata hujaanza.
  5. Usijifunze kutokana na makosa yako, badala yake jifunze kutokana na mafanikio yako. tumezoea kuambiwa jifunze kutokana na makosa, lakini hilo halisaidii sana. jifunze kutokana na mafanikio yako, hata kama ni madogo sana, utajua njia sahihi ya kufanya ili ufanikiwe tena.
  6. Huhitaji kushindwa ndiyo uweze kufanikiwa. Kushindwa kumekuwa kunatukuzwa sana, kwamba ukishindwa ndiyo utafanikiwa. Mafanikio yanakaribisha mafanikio zaidi kuliko kushindwa. Hivyo kazana upate hata mafanikio kidogo na yatakuwezesha kufanikiwa zaidi.
  7. Kupanga ni kubashiri. Chochote unachopanga kwa ajili ya kesho au siku zijazo ni kujifurahisha tu, kwa sababu hujui chochote kitakachotokea kesho au siku zijazo.
  8. Achana na kazi za ubashiri, huhitaji kuwa na mpango wa muda mrefu ujao, chagua nini utafanya juma linalokuja na fanya hicho. Kadiri unavyokwenda utakutana na mambo tofauti ambayo huenda hukuyategemea, utabadilika kadiri itakavyohitajika.
  9. Siyo lazima kila biashara ikue ndiyo ionekane imefanikiwa. Mafanikio ya biashara ni kuifanya kwa namna ambayo inatatua tatizo la mteja na wewe mwendeshaji wa biashara kuridhika na namna biashara inavyoenda.
  10. Siyo lazima kila biashara iwe na matawi ndiyo ionekane kufanikiwa. Mfano chuo kikuu cha Havard ni chuo kikubwa na chenye mafanikio makubwa sana duniani, lakini kipo kimoja tu. Ingekuwa rahisi kusema wangeweza kufungua matawi dunia nzima, lakini hiyo siyo njia sahihi kwao kupima mafanikio.
  11. Kukimbilia kuajiri haraka ndiyo kinachoua biashara nyingi. Watu wengi wanakimbilia kukua na kujikuta wana gharama kubwa za kuendesha biashara kuliko wanavyoweza kumudu. Kua taratibu, fanya kile chenye uhitaji na siyo kwa sababu wengine wanasema ufanye.
  12. Huhitaji kuweka muda wako wote wa siku kwenye biashara yako, unahitaji muda wa kupumzika. Hata kama unaipenda sana biashara yako na una mengi ya kufanya, kukesha kila siku kutaleta madhara makubwa kuliko mafanikio.
  13. Neno mjasiriamali limeshatumiwa sana mpaka limekosa maana sasa. Maana kila mtu anajiita mjasiriamali kwa sababu tu kuna kitu anauza. Badala ya kujiita mjasiriamali, jiite mwanzilishi, anzisha biashara na ikuze, hiyo ndiyo njia sahihi kufanikiwa.
  14. Acha alama hapa duniani. Tumia biashara yako kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi mpaka mteja mwenyewe aseme kitu hiki kimefanya maisha yangu kuwa bora zaidi.
  15. Kuna panapowasha. Biashara nzuri kwako kuanzisha ni kutatua tatizo ambalo wewe mwenyewe linakusumbua, kisha kuangalia watu wengine ambao linawasumbua na kuwapatia suluhisho lililokusaidia wewe.
  16. Uzuri wa kutatua tatizo ulilonalo ni kwamba kwanza utapenda, na pili hutachoka, kwa sababu huenda ni kitu utakachofanya kwa maisha yako yote.
  17. Kama kuna kitu ambacho unakitaka hasa, muda wa kukifanya utaupata, hata kama umebanwa kiasi gani. Hivyo kama unajiambia huna muda, unachosema ni kwamba siyo kitu unachotaka hasa.
  18. Chagua kitu utakachosimamia, na simamia kitu hicho. Kuna watu watakupinga, lakini unahitaji kusimama kwenye kile unachoamini. Na hii ni njia nzuri ya kutengeneza wateja ambao ni mashabiki wako, kwa sababu wanasimamia kile unachosimamia.
  19. Kuwa tayari kupoteza baadhi ya wateja pale unaposimamia kitu fulani. Siyo lazima kila mtu awe mteja wako, hivyo usivunje msimamo wako ili kupata wateja zaidi.
  20. Tupo kwenye uchumi wa huduma, kinachofanya biashara yoyote ifanikiwe sasa, ni ubora wa huduma ambayo biashara hiyo inatoa. Hata kama biashara inauza kitu cha kawaida, bila ya huduma bora, haiwezi kufanikiwa.
  21. Njia bora ya kuanza biashara yako ni kwa fedha zako mwenyewe, au kuanzia chini kabisa. Kuanza na fedha za wengine, kama mkopo au hata wawekezaji, ni njia ambayo inakupa ukomo kwenye mengi. Maana huwezi kufanya majaribio na fedha za wengine.
  22. Hakuna ubaya kuanza biashara kwa ubahili, hata kama huna vingi unavyopaswa kuwa navyo, kama unaweza kutatua tatizo la mteja, anzia hapo, kisha utaendelea kukua kadiri unavyokwenda. Kama huna ofisi anzia nyumbani kwako, kama huna kompyuta tumia simu yako. Kama huwezi kuajiri fanya kila kitu mwenyewe.
  23. Kama biashara haina njia ya kuelekea kwenye faida hiyo siyo biashara, bali ni hobi. Ni kitu unachopenda kufanya unapokuwa na muda. Kama unaingia kwenye biashara, lazima uwe na mpango wa faida ambao unafanya kazi, la sivyo hutadumu kwenye biashara hiyo.
  24. Usiingie kwenye biashara na mkakati wa kutoka, bali ingia ukiwa na mkakati wa kung’ang’ana mpaka ufanikiwe. Wengi huingia kwenye biashara wakiwa wameshajiambia kama itashindwa basi nitaenda kwenye biashara hii, hapo wanajiandaa na kushindwa, na wengi hushindwa.
  25. Kama umeingia biashara kwa sababu ni tatizo ulilonalo na umeweza kulitatua, huna haja ya kuondoka kwenye biashara hiyo. Kama biashara unaipenda, na inatengeneza faida, huna haja ya kutafuta njia ya kuuza biashara hiyo na kupata faida kubwa. Wengi waliouza biashara zao kwa faida kubwa wanaishia kuwa na maisha ambayo siyo ya furaha kwao. Kama unaipenda biashara yako kweli, na kama inatengeneza faida, ifanye mpaka siku unakufa.
  26. Kinachoua biashara nyingi ni uzito. Biashara huwa zinaanza zikiwa nyepesi, halafu zinaanza kubeba mizigo ya mikataba, wafanyakazi wengi, mikutano, michakato mbalimbali, siasa za ofisini na kadhalika. Kadiri biashara yako inavyokuwa na mzigo mwepesi, ndivyo inavyokua kwa kasi.
  27. Biashara kubwa zinachukua muda mrefu sana kufanya mabadiliko muhimu, kwa sababu yanapitia ngazi mbalimbali. Biashara ndogo ina faida ya kuweza kufanya maamuzi haraka pale fursa inapojitokeza na kuweza kunufaika nayo. Mara zote fanya maamuzi kama biashara ndogo hata kama biashara ni kubwa.
  28. Tumia uhaba kama sababu ya kufanya zaidi. Watu wengi hutumia uhaba kama sababu ya kutokufanya, lakini wewe unahitaji kutumia uhaba kama sababu ya kufanya zaidi. Kama una muda mfupi, basi unautumia vizuri badala ya kuupoteza. Kama huna wafanyakazi wengi basi unafanya yale muhimu tu na kuachana na mengine yasiyo muhimu.
  29. Nusu ya vitu unavyofanya sasa huhitaji kuvifanya, hata kama unavipenda sana. Cha kufanya orodhesha vitu vyote unavyofanya, kisha acha kufanya nusu ya vile unavyofanya sasa. Utaongeza ufanisi na utaweza kukua zaidi.
  30. Anzia kwenye kitovu. Watu wengi wanapopata wazo la kufanya kitu, huwa wanaanza kufikiria mambo makubwa na magumu, na mwishowe wanakata tamaa. Kama unataka kufanya kitu chochote, anzia kwenye kitovu na hapo utaweza kuona hatua rahisi zaidi za kuchukua. Kwa mfano kama unataka kuanzisha mgahawa, unaweza kuanza kufikiria kuhusu upatikanaji wa bidhaa utakazotumia, eneo unalofanyia, wapishi wazuri na kadhalika. Lakini ukianzia kwenye kitovu, ambacho ni unahitaji kuwa na chakula kizuri kwa wateja wako, mengine yote ni rahisi kufuata.
  31. Maelezo yasikusumbue mwanzoni, angalia kipi unachotaka kufanya na utakifanyaje, maelezo mengine unaweza kuyapuuza kwa mwanzoni. Kama unajenga nyumba, huanzi kufikiria kuhusu taa za aina gani utanunua, unaanza kufikiria kuweka msingi na kusimamisha jengo. Taa za aina gani ni kitu cha baadaye sana, ambacho hakipaswi kukusumbua mwanzoni.
  32. Fanya maamuzi wakati unapokutana na hitaji la kufanya maamuzi. Usijiambie wacha nifikiri nitaamua baadaye. Kama kitu ni muhimu fanya maamuzi sasa, au hutayafanya kabisa. Maamuzi yanayosogezwa mbele ni maamuzi ambayo yamekuwa hayafanywi.
  33. Usiogope kukosea pale unapochagua kufanya maamuzi. Ni bora ufanye maamuzi ukosee, kwa sababu utarekebisha makosa yako, kuliko kutokufanya maamuzi kabisa.
  34. Mara zote angalia kitu gani unaweza kupunguza, vitu unavyopunguza ndiyo vinafanya kitu kiwe kizuri. Chukulia chochote unachofanya kama mchonga vinyago, kila gogo lina kinyago ndani yake, ni aina gani ya kinyago utategemea na vitu gani vitaondolewa kwenye gogo hilo, na siyo kuwekwa. Hata kwenye uandishi, ubora wa uandishi siyo nini kimewekwa, bali nini kimetolewa. Kila mara angalia kitu cha kuondoa na kupunguza, ili ubaki na vile vilivyo bora kabisa.
  35. Kama kuna tatizo, angalia nini cha kupunguza. Mazoea ya wengi ni pakiwa na tatizo basi wanaongeza vitu zaidi, watu zaidi, fedha zaidi, muda zaidi na wanaishia na kuwa na tatizo kubwa zaidi. Kama kuna tatizo angalia kipi cha kupunguza, na utaweza kutatua tatizo hilo.
  36. Weka nguvu zako kwenye vitu ambavyo havitabadilika. Watu wengi huwa wanakazana kukimbizana na vitu vinavyopita, fursa mpya, fasheni na habari mpya ya mjini. Wewe kazana na vile ambavyo siyo vya kupita, na biashara yako itakuwa imara. Achana na vitu ambavyo watu wanataka sasa, kazana na vitu ambavyo watu wataendelea kuhitaji miaka kumi ijayo.
  37. Kuna kitu kimoja pekee muhimu kwenye biashara, jinsi gani ya kupata wateja na kutengeneza fedha. Mengine nje ya hapo ni kelele na usumbufu. Usisumbuke na mambo ambayo hayakupeleki kwenye eneo hilo muhimu.
  38. Tumia kile ulichonacho sasa kufanya unachotaka kufanya. Watu wengi wamekuwa wanajikwamisha kwa sababu hawana vifaa vizuri. Kinachohitajika ni ufanye kitu na siyo vifaa. Kama unataka kutengeneza video na huna kamera kubwa, tumia simu yako, ujumbe unaotaka kutoa ni muhimu kuliko njia ya kuutolea.
  39. Uza masalia ya bidhaa au huduma yako. Fundi seremala anapotengeneza thamani kwa kutumia mbao, huwa anabaki na masalia kama maranda, vipande vya mbao na kadhalika. Vyote hivyo vinaweza kuuzwa kwa wenye uhitaji. Kwenye biashara unayofanya, kuna masalia ambayo unaweza kuyauza na ukatengeneza fedha pia. Inawezekana masalia yako ni kile ulichojifunza kwenye kuanzisha biashara yako, unaweza kuweka kwenye kitabu na ukauza kitabu hicho.
  40. Vitu vingi unavyofikiri unahitaji ili kuanza biashara wala huvihitaji sana. Jiulize swali hili, kama ungepaswa kuanza biashara yako ndani ya wiki mbili, vitu gani ungeachana navyo ambavyo sasa hivi unavifikiria. Hivyo ndiyo unapaswa kuviacha na kuanza.
  41. Kwenye biashara kuna njozi nyingi sana za makubaliano. Watu wamekuwa wanapoteza muda kwenye ripoti ambazo hakuna hata anayezisoma. Kama kuna kitu unahitaji kukielezea, huhitaji kuwa na ripoti kubwa, unahitaji kuelezea kitu hicho kwa msingi na kwa namna ambayo kila mtu anaweza kuelewa.
  42. Usumbufu unapunguza sana ufanisi kwenye kazi. Watu wengi inabidi wafanye kazi kwa muda mrefu na kwa siku zote za wiki kwa sababu hawawezi kutumia vizuri muda wa kawaida wa kazi, wanakubali usumbufu uvuruge kazi zao.
  43. Usumbufu mwingi kwenye kazi unatokana na mawasiliano na vikao. Mawasiliano ya simu, email na hata mitandao ya kijamii inawafanya watu washindwe kuweka muda kwenye kazi zao. Mikutano na vikao vingi ambavyo watu inabidi wahudhurie siyo muhimu na havihitaji watu wengi, lakini vinaishia kupoteza muda wa wengi.
  44. Tengeneza sheria ya kuwa na muda wako. Labda kwenye siku yako, unatenga masaa ya kazi ambayo huwezi kusumbuliwa. Ukiweza kupata masaa manne ya kazi ambayo husumbuliwi kila siku, utaweza kufanya makubwa kuliko mtu anayefanya kazi usiku na mchana na mpaka mwisho wa wiki.
  45. Vikao ni sumu kwenye kazi na biashara. Kwa sababu huwa vinahusu vitu visivyo muhimu, vinakuwa na watu wengi wasiohusika, kila mtu anataka aongee hata kama hana muhimu la kuongea na mara nyingi vikao huwa vinaenda nje ya mada iliyopangwa. Epuka sana vikao kwenye kazi na biashara zako, utaokoa muda mwingi na kuweza kufanya mengi.
  46. Kama kuna ulazima wa kuwa na vikao, basi hakikisha kwamba; tenga muda wa kikao na isizidi hata dakika moja, muda ukiisha kikao kinaishia hapo, hata kama hamjafikia maamuzi, kikao kihudhuriwe na watu wachache, wale ambao ni muhimu hasa, ajenda ziwe wazi na zifuatwe na kikao kifanyike eneo la tatizo au tukio, na watu wawe wamesimama.
  47. Matatizo mengi yanaweza kutatuliwa kwa njia rahisi sana, kama utaacha kutafuta njia ngumu za kuyatatua.
  48. Usiogope kuacha kitu pale unapoona hakikupi matokeo uliyotaka. Watu wengi huwa wanafikiria kuacha ni kushindwa. Siyo sahihi, unaweza kuacha kitu ambacho hakifanyi vizuri na kufanya kingine ambacho kitakuwezesha kufanikiwa zaidi.
  49. Pata muda wa kutosha wa kupumzika, biashara yako inakuhitaji uwe na nguvu ya mwili na akili iwe vizuri, vitu ambavyo unavipata kama utapumzika.
  50. Usikadirie chochote, weka juhudi kwa kadiri unavyoweza, lakini usilazimishe matokeo unayotaka wewe.

Rafiki, kwenye kitabu hiki nimeorodhesha mambo 105 ya jinsi ya kuifanya  biashara yako kwa utofauti na ukafanikiwa sana. Nimekushirikisha hayo 50 hapo, na kama utayafanyia kazi, basi utaweza kupiga hatua sana kwenye biashara yako. Pata muda usome kitabu hiki, kitakusaidia sana kuendesha biashara yako kwa viwango vyako mwenyewe.

#2 MAKALA YA JUMA; DUNIA HAINA UHABA WA FEDHA.

Kila siku ya juma kunakuwa na makala mpya kwenye mtandao wa AMKA MTANZANIA. Hivyo ni jukumu lako kuingia kwenye www.amkamtanzania.com kila siku na utakutana na makala mpya ya kukupa maarifa na hamasa ya kufanikiwa zaidi.

Juma hili moja ya makala muhimu sana niliyokushirikisha ni kuhusu uhaba wa fedha. Watu wengi wasiokuwa na fedha wamekuwa wakiamini hawana fedha kwa sababu kuna uhaba wa fedha. Kitu ambacho siyo sahihi kabisa. Hakuna uhaba wa fedha kwenye hii dunia. Ila kuna uhaba wa vitu vitano ambavyo nimevieleza kwenye makala hii, fungua kusoma; Dunia Haina Uhaba Wa Fedha, Bali Ina Uhaba Wa Vitu Hivi Vitano Ambao Unawazuia Watu Kupata Fedha.

Kuna makala nyingine nilikushirikisha ya maswali mawili muhimu ya kujiuliza kabla hujaingia kwenye biashara. Kama unapanga kuingia kwenye biashara, au hata kama tayari upo kwenye biashara, hakikisha umesoma makala hii. Kama hujaisoma, unaweza kuisoma hapa; Maswali Mawili (2) Muhimu Sana Ya Kujiuliza Kabla Hujaingia Kwenye Biashara Yoyote Ile

cropped-mimi-ni-mshindi

#3 TUONGEE PESA; SHERIA YA SIKU 30 KWENYE FEDHA.

Moja ya tatizo kubwa ambalo watu wanalo kwenye fedha ni kushindwa kudhibiti matumizi. Watu wanapokuwa na fedha, na wakakutana na kitu kizuri, wanajikuta wameshanunua.

Ndiyo maana watu wanaishia kuwa na nguo ambazo hawazivai, vitu ambavyo hawavitumii, lakini wamenunua. Ukiwauliza kwa nini walinunua hata hawawezi kukupa jibu la wazi. Wengine watakuambia ilikuwa rahisi na wasingeweza kupata kwa bei rahisi vile. Wengine watakuambia wanajua watakuja kuhitaji kitu hicho siku moja.

Haijalishi unajifariji kwa maneno gani, kama umenunua kitu ambacho hukitumii sana, umepoteza fedha. Au kama umenunua kitu, lakini inakulazimu ukitumie ili usijione umepoteza fedha, jua umeshapoteza fedha.

Sasa, ipo sheria inayoweza kukusaidia usirudie tena makosa uliyofanya huko nyuma ya kununua kitu ambacho hukitumii. Sheria hiyo ni sheria ya siku 30.

Sheria hii inasema kwamba, kama umekutana na kitu na ukajishawishi unahitaji kukinunua, usikinunue hapo hapo. Badala yake andika mahali kwamba unataka kununua kitu hicho, kisha subiri kwa siku 30 kabla hujakinunua. Sasa kama siku 30 zitaisha na bado ukawa unauhitaji mkubwa wa kitu hicho, au hata siku 30 hazijaisha uhitaji unakuwa mkubwa mno la sivyo maisha hayawezi kwenda, nunua kitu hicho.

Rafiki, kwa sheria hii, usijidanganye kwamba hii ni bei rahisi na hutapata tena, au kitu hicho ni cha mwisho na hakitapatikana tena. Sheria ni moja, subiri siku 30 zipite na utanunua.

Kitu ambacho utanufaika nacho kwenye sheria hii ni kwamba baada ya siku tatu kupita, wala hata hutakumbuka kama ulipanga kununua kitu hicho.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; NJIA PEKEE YA KUKUTANA NA MIMI KOCHA WAKO.

Kama umekuwa unafuatilia kazi zangu kwa karibu, na zimekuwa zinakunufaisha, basi kuna vitu mpaka sasa utakuwa unaviona kupitia kazi zangu ambavyo hukuwa unategemea. Utakuwa hunioni kwenye mitandao ya kijamii, hunisomi kwenye magazeti, hunioni kwenye tv wala kunisikia kwenye redio. Pia utakuwa umetamani sana tukutane lakini hilo halifanikiwi. Siyo kwamba hayo yote hayawezekani, bali naweka vipaumbele kwenye kila ninachofanya. Najua muda wangu kwa siku ni mchache na nina mengi ya kufanya. Hivyo neno la kwanza linalotoka kwangu ninapoulizwa au kuombwa chochote ni HAPANA. Na hapo ndipo lazima mtu aeleze kwa nini ni muhimu sana niache kufanya vitu vingine na nikubaliane na kile anataka yeye.

Kwa kuwa upatikanaji wangu ni mdogo sana, basi nimekuwa naendesha semina moja tu kwa mwaka ya kukutana ana kwa ana. Ni semina moja pekee ambapo utakutana moja kwa moja na mimi kocha wako, pamoja na wanamafanikio wengine waliopo kwenye safari ya mafanikio.

Hivyo ni nafasi ambayo mtu yeyote anayetaka kupiga hatua kwenye maisha yake, hapaswi kuikosa. Na kwa mwaka huu 2018, semina ni tarehe 03/11/2018. Ukikosa siku hii moja, utasubiri tena mpaka mwaka 2019.

Hivyo nakupa nafasi ya kujihakikishia nafasi ya kushiriki semina hii, kwa kutuma majina yako na namba ya simu na kueleza kwamba utashiriki semina. Ujumbe unatuma kwa namba 0717396253 kwa ujumbe wa kawaida au wasap.

Ada ya kushiriki semina hii ni tsh laki moja (100,000) na mwisho wa kulipa ada ni tarehe 31/10/2018. Unaweza kulipa ada hii kidogo kidogo, kila siku, kila wiki na kila mwezi kabla ya kufika tarehe hiyo ya mwisho.

Unaponitumia ujumbe pia nijulishe mpango wako wa malipo unafanyaje ili niweze kukupa nafasi ya kulipia na uweze kushiriki semina hii muhimu sana kwako kwa mwaka huu 2018.

Karibu sana tukutane pamoja tarehe 03/11/2018 tupeane mikakati ya mafanikio tunayokwenda kufanyia kazi kwa mwaka wa mafanikio 2018/2019.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; TATIZO SIYO NDOTO.

‘There are those who dream and wish and there are those who dream and

work.’ – Jeune.E. McIntyre.

Siku za nyuma, wakati ambapo maarifa yalikuwa magumu kupatikana, watu wengi walikuwa wanazuiwa na ndoto kufanikiwa. Wengi walifikiria kidogo sana na ndiyo maana waliishia kuwa na maisha ya kawaida.

Hivi unajua kwamba kabla ya Colombus kuzunguka dunia watu walikuwa wanaogopa kwamba wakienda mbali na pale walipo watafika ukingoni mwa dunia na kuanguka? Ona jinsi watu walikuwa na ndoto ndogo.

Na je unajua kabla ya Hendry Ford kugundua magari, watu waliogopa kwamba ukitumia chombo cha usafiri kinachoenda kwa kasi ya zaidi ya maili 30 kwa saa damu itaacha kuzunguka mwilini na utakufa? Ona jinsi ukosefu wa maarifa uliwafanya wengi kuwa na ndoto ndogo.

Lakini siyo leo, leo maarifa yamejaa kila kona, simu ndogo tu ya mkononi inaweza kukupa maarifa mengi kuliko aliyokuwa nayo raisi wa Marekani miaka 50 iliyopita.

Sasa hivi kila mtu anaweza kuwa na ndoto kubwa, na ni rahisi kusema, nataka kufika hapa, nataka kufika pale.

Lakini kinachowatofautisha watu sasa, yaani wale wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni utendaji, yaani kuchukua hatua.

Kama anavyotuambia Jeune, kuna wanaokuwa na ndoto kubwa na kuishia kutamani kufikia ndoto hizo, halafu kuna wale wanaokuwa na ndoto kubwa na kuanza kufanyia kazi ndoto hizo. Sihitaji kukuambia nani atafanikiwa katika hao wawili, najua unajua na hivyo ninachokuambia ni nenda kaweke kazi kama kweli unataka kufikia ndoto kubwa ulizonazo.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu

Usomaji