Rafiki yangu mpendwa,

Fedha ni lugha ambayo kila mtu anaielewa, bila ya kujali umri, rangi, kabisa au jinsia. Kila mtu anaielewa fedha kwa sababu kitu pekee ambacho mtu anaweza kupata bila ya kulipia ni pumzi, na hapo ni kama hajapatwa na maradhi makubwa.

Pamoja na umuhimu huu mkubwa wa fedha kwenye maisha ya kila mtu, bado watu wengi wanaishi maisha ya kuteseka sana. Wengi wanakazana sana kuzitafuta fedha lakini hawazipati. Na hata zile kidogo wanazopata, zinawapotea kabisa, wasijue hata zimeenda wapi.

Hapa ndipo wengi huamini kwamba dunia ina uhaba wa fedha, na hivyo wengi wametengwa kwenye fungu la kukosa huku wachache wakihodhi fedha chache zilizopo. Wale ambao hawana fedha, wanafikiri kinachowakosesha wao fedha ni wale wachache wenye fedha nyingi.

Na pale inapokuja kwamba wenye fedha wanazidi kupata fedha nyingi zaidi, huku wale ambao hawana wakiendelea kukosa, imani ya uhaba wa fedha inakuwa kubwa sana kwa wengi ambao hawana fedha.

Lakini kiukweli na kiuhalisia, dunia haina uhaba wa fedha. Na ndiyo maana utajiri wa dunia umekuwa unaendelea kuongezeka siku hadi siku. Hii ina maana kwamba kama fedha zilizopo sasa haziwatoshi wale wanaozitaka, nyingi zaidi zitachapishwa kukidhi mahitaji ya wengi.

KWA NINI SIYO TAJIRI

Sasa kama dunia haina uhaba wa fedha, ni kitu gani kinawafanya wengi wasipate fedha wanazotaka?

Kuna uhaba wa vitu hivi vitano ambao ndiyo unapelekea wengi wasipate fedha wanazotaka.

Moja; uhaba wa mipango dhabiti.

Watu wengi huwa hawana mipango dhabiti ya kupata fedha na utajiri. Mwulize mtu yeyote anayekuambia hana fedha, anataka fedha kiasi gani na baada ya muda gani. Ataishia kukuambia anataka fedha nyingi. Sasa kama sasa hivi una elfu kumi, elfu 20 ni fedha nyingi kwako. Je unafikiri utapata fedha nyingi kwa kusema unataka fedha nyingi? Hilo halitotokea.

Unahitaji kuwa na mpango dhabiti wa kupata fedha, lazima ujue kiasi gani cha fedha unataka, na utakipata baada ya muda gani. Pia lazima ujue ni nini unapaswa kutoa ili kupata fedha hizo unazotaka.

Safari ya kwanza kwenye kupata fedha ni kuamua kiasi cha fedha unachotaka, muda utakaotumia kupata fedha hizo na kile utakachotoa ili upate fedha hizo. Ruka hatua hii na utazunguka maisha yako yote usijue hata ni nini unafanya.

Mbili; hamasa.

Safari ya kupata fedha unazotaka siyo rahisi, ina magumu, vikwazo na changamoto. Hivyo bila ya hamasa, safari hiyo itakuwa ngumu na utakata tamaa.

Unahitaji kuwa na hamasa ya kuweza kufuata mpango ulioweka, licha ya kukutana na nyakati ngumu kwako. Unahitaji kuweza kujisukuma zaidi, kwenda hatua ya ziada ili kuweza kupata fedha unazotaka.

SOMA; Faida Ni Bora Kuliko Mshahara; Falsafa Kumi (10) Za Jim Rhon Zitakazokuwezesha Kupata Mafanikio Makubwa Sana.

Tatu; ujasiri.

Ujasiri ni kitu kingine ambacho kimeadimika kwa wengi na kinawazuia wasipate fedha wanazotaka. Ujasiri unahitajika sana pale unapojitoa kwamba unataka kupata fedha zaidi. Kwa sababu wengi watakupinga, wengine watakuona wewe ni mbaya na wengine watakukatisha tamaa.

Lazima uwe jasiri, uweze kusimamia kile unachoamini na kile unachotaka, bila ya kutetereka.

Pia pale unapowataka watu wakulipe zaidi ya walivyozoea kukulipa, unahitaji ujasiri. Wengi huwa wanahofia hapo na kuendelea kupokea kiasi kidogo walichozoea kupewa.

Ujasiri utakuwezesha kutaka fedha zaidi na kuwataka watu wakulipe zaidi kulingana na thamani unayotoa.

Nne; kuchukua hatua.

Watu wengi huwa wanapanga na wanajiambia wana ujasiri, lakini inapofika kwenye kuchukua hatua, wanapooza. Wengi hawachukui hatua kabisa, au hatua wanazochukua haziendani na kiasi cha fedha wanachotaka.

Kwa mfano, huwezi kupata fedha nyingi unazojiambia unataka kupata, kama unafanya kazi masaa 8 kwa siku na siku 5 kwa wiki, huku ukipoteza jioni zako na siku za mwisho wa wiki kwa mambo ambayo hayakuingizii fedha.

Unahitaji kuweka muda wako mwingi kwenye shughuli zinazokuingizia fedha. Unahitaji kupima kila kitu kwa kiasi cha fedha ambacho unakipata kabla hujaanza kufanya.

Ndiyo kuna watu watakuona unapenda fedha sana na hujali mengine, na hapo ndipo ujasiri unapohitajika. Kwa sababu kama unataka kumfurahisha kila mtu, jua hakuna hatua kubwa utakayoweza kupiga.

SOMA; Njia Nne Za Kuleta Mabadiliko Ya Kudumu Kwenye Maisha Yako, Yatakayokufikisha Kwenye Mafanikio Makubwa.

Tano; ufuatiliaji.

Watu wengi wanachukua hatua mara moja, hawapati wanachotaka kisha wanakata tamaa, wanaona hawawezi tena kupata wanachotaka.

Hayo ni makosa makubwa sana kwenye kutaka kupata fedha zaidi. Mpaka watu wawe tayari kukupa fedha zao ambazo wamezipata kwa shida, wanahitaji kujihakikishia kwamba kile unachowaambia ni kweli na kitawasaidia. Hivyo hilo linahitaji muda na linahitaji kuwapa elimu ya kuwatosha.

Hivyo kama unataka kupata fedha, lazima uwe na ufuatiliaji wa karibu sana kwa wale ambao unataka wakupe fedha. Kama unafanya biashara, wafuatilie kwa karibu sana wateja wako. Mteja amekuambia atanunua, usisubiri mpaka arudi mwenyewe, kwa sababu hatorudi. Badala yake mfuatilie na mkumbushe kwamba alisema atarudi.

Fuatilia sana ili kupata fedha unayotaka, usifanye mara moja au mbili na kusema haiwezekani, fuatilia kwa muda mrefu na mwisho wa siku utapata kile unachotaka.

Dunia haijawahi kuwa na uhaba wa fedha wala hautakuja kutokea, bali uhaba wa fedha ni matokeo ya uhaba wa mipango, hamasa, ujasiri, kuchukua hatua na kufuatilia. Fanyia kazi vitu hivi vitano, na fedha hazitakuwa tena tatizo kwako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL