Rafiki,

Kuna watu ambao huwa wanajisikia tu vibaya pale mtu anapoanza kuzungumzia fedha. Wanaona mtu huyo ana tamaa za fedha na pia ni mwovu na asiyejali kuhusu wengine.

Kitu ambacho nimejifunza kuhusu tabia za watu na fedha ni hiki, kwenye eneo la fedha, ndipo unafiki wa binadamu ulipolala.

Watu wengi ambao hawana fedha za kuwawezesha kuyaendesha maisha yao kwa namna ambayo wanataka wao, huwa wanajidanganya kwamba hata hivyo fedha siyo muhimu sana kwao. Kwamba wana furaha na maisha yao vile yalivyo na wale wenye fedha hawana furaha kama wao.

FEDHA KWA BLOG

Hivi mtu unawezaje kupima furaha ya wengine kwa kujilinganisha na furaha yako? Hapa ndipo unafiki mkuu wa fedha unapoanzia.

Unafiki mwingine ni pale watu wanapojiambia fedha hainunui furaha, kwamba wenye fedha hawana furaha kama wasio na fedha. Nasema huu ni unafiki kwa sababu kwa nini ulinganishe fedha na furaha, je kutokuwa na fedha ndiyo kunanunua furaha? Na pia nasema ni unafiki kwa sababu kauli za aina hii zimekuwa zinatolewa na wale ambao hawana fedha.

Rafiki, kama umesoma mpaka hapa, ni imani yangu kwamba fedha ni kitu ambacho unakipa kipaumbele kwenye maisha yako, na upo tayari kuachana na unafiki unaowapooza wengi ambao wamechagua kuishi maisha ya chini ya viwango vyao.

Sasa leo nataka tujadili tatizo kubwa la fedha ambalo unalo, na jinsi ya kulitatua ili kuweza kuwa na maisha bora kama unavyotazamia.

KWA NINI SIYO TAJIRI

Tatizo kubwa la fedha ambalo wengi wanalo, na ambalo hata wewe unalo, ni HUNA FEDHA ZA KUTOSHA. Ndiyo, huna fedha za kutosha na hili ndiyo linayafanya maisha yako yawe magumu.

Najua umejifunza, kwa njia ya maumivu kwamba kipato chako hakijawahi kutosha, kwamba kadiri kipato kinavyoongezeka, ndivyo matumizi nayo yanaongezeka.

Ulipokuwa unaingiza kipato kidogo ulifikiri kipato kikiongezeka basi maisha yako yatakuwa mazuri kwa kuweza kupata chochote unachotaka. Lakini hicho siyo kilichotokea. Kipato kimeongezeka na mahitaji nayo yameongezeka, pia matatizo yamekuwa makubwa zaidi.

Wengi walifikiri kwa kuwa na fedha nyingi basi hakuna matatizo yatakayowasumbua, wanachojifunza ni kadiri fedha zinavyokuwa nyingi, ndivyo matatizo nayo yanakuwa makubwa zaidi.

SOMA; Dunia Haina Uhaba Wa Fedha, Bali Ina Uhaba Wa Vitu Hivi Vitano Ambao Unawazuia Watu Kupata Fedha.

Hivyo rafiki yangu, hicho ndiyo kiini cha matatizo yako yote ya kifedha, huna fedha za kutosha. Kama ungekuwa na fedha za kutosha, sehemu kubwa ya matatizo yanayokukabili sasa yangepata suluhisho, na hata yakiibuka makubwa zaidi utaweza kuyasuluhisha.

Kama ungekuwa na fedha za kutosha, huenda usingegombana na watu wengi unaogombana nao, usingewachukia baadhi ya watu unaowachukia sasa. Unapokosa fedha za kutosha, ni rahisi kumwona kila mtu ni adui yako.

Sasa rafiki, nakwenda kukupa njia ya kutatua tatizo hili kubwa la kifedha ulilonalo.

Na njia hiyo siyo rahisi wala haihitaji haraka, ila kila mwenye utulivu anaweza kuifanyia kazi.

Njia pekee itakayoweza kukuondoa kwenye tatizo kubwa la fedha kutokutosha ni KUTENGENEZA MFUMO WA KULIPWA UKIWA UMELALA.

Hapa simaanishi kwamba uache kufanya kazi, bali ninamaanisha uwe na njia ambayo utaendelea kulipwa, iwe unafanya kazi au la. Yaani lazima uwe na mfumo unaoingiza fedha. Kwa maneno mengine tunaweza kusema uwe na mashine ya kuchapa fedha muda wote wa maisha yako.

Ukitegemea kile kipato ambacho kinaingia baada ya wewe kufanya kazi, hata kiwe kikubwa kiasi gani, hakiwezi kukutosha. Kwa sababu kipato hiki lazima kitakuwa na ukomo. Lakini ukitengeneza mfumo ambao unaingiza kipato iwe unafanya kazi au la, hujiwekei ukomo kwenye kipato chako. Baada ya muda unajikuta una fedha za kutosha kuyaendesha maisha yako kwa jinsi unavyotaka na huna wasiwasi wala mahangaiko.

Kipato cha moja kwa moja ni kama mshahara au faida unayopata kwenye biashara unayoiendesha wewe mwenyewe. Hivi ni vipato ambavyo kadiri unavyotaka zaidi, ndivyo unavyoingia kwenye utumwa zaidi kwa sababu vinahitaji muda wako na nguvu zako.

Kipato kisicho cha moja kwa moja, ambacho kinaweza kuingia hata kama hufanyi kazi ni faida unayopata kwenye uwekezaji na biashara inayojiendesha yenyewe bila ya wewe kuwepo. Hapa kipato kinaingia hata kama wewe hufanyi kazi moja kwa moja.

Uwekezaji na mfumo wa biashara inayojiendesha yenyewe ni vitu unavyoweza kuanza kuvifanya mara moja kwenye maisha yako, na kama hujaanza kuvifanya basi nashauri uanze mara moja, tena uanze leo.

Anza kuwekeza kidogo kidogo, kwenye kila kipato unachoingiza, sehemu ya kipato hicho itenge kwa ajili ya uwekezaji. Na unaweza kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali, kuanzia masoko ya mitaji, vipande, hatifungani, pia kuwekeza kwenye ardhi, majengo na hata biashara za wengine.

Pia anza biashara ambayo utaitengeneza kwa mfumo wa kuweza kujiendesha yenyewe mbeleni. Mwanzoni inaweza kukutegemea, lakini malengo yako makubwa ya mbeleni ni biashara hiyo iweze kujiendesha yenyewe.

Anza vitu hivi viwili mara moja ili kutatua changamoto ya kipato inayokusumbua. Na kama utahitaji msaada wowote katika hayo mawili ya kujitengenezea kipato kisicho na ukomo, basi karibu sana ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA, ambapo tutakuwa pamoja, tutakuwa karibu na kujifunza mengi zaidi.

MUHIMU; Kwenye KISIMA CHA MAARIFA, kuna semina mbili ambazo unapaswa kuzisoma ili kufanikiwa kwenye hayo mawili niliyokushirikisha, ya kwanza ni ELIMU YA MSINGI YA FEDHA na ya pili ni UKUAJI WA BIASHARA. Ukijiunga na KISIMA CHA MAARIFA, nitakupa masomo ya semina hizo na utaweza kujifunza na kuanza kuchukua hatua mara moja ili kufanikiwa. Jiunge leo na uanze kushika hatamu ya maisha yako.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu