2501; Kama nafsi inakataa, isikilize.

Kuna wakati unaweza kuwa na fursa fulani mbele yako, fursa ambayo inaonekana ni nzuri kabisa, lakini nafsi yako inakataa kabisa kuikubali fursa hiyo.

Mara nyingi hili hutokes pale unapohitaji kujihusisha na watu fulani. Labda ni kwenye kazi au biashara. Kwa nje wanaonekana ni watu wazuri lakini nafsi yako inakataa kufanya nao kazi.

Ukiipuuza nafsi yako kwenye hilo na ukaendelea kufanya, unakuja kugundua baadaye jinsi ambavyo umefanya makosa kukubali hilo.
Wanakuja kuwa ni watu ambao ni wasumbufu na wanaokuletea ugumu mkubwa katika kutekeleza kile ulichopanga.

Lakini kuna changamoto hapo, utajuaje ni nafsi inakuambia au hofu inakuzuia? Maana unapotaka kufanya mapya na makubwa, hofu pia hujitokeza na kuwa kikwazo.

Tofauti ya nafsi na hofu ni nafsi inaanzia rohoni na hofu inaanzia akilini.
Kama unapata mkwamo baada ya kufikiria sana na kuchambua kwa kina kisha ukasita, hiyo ni hofu na hupaswi kuiruhusu iwe kikwazo.

Lakini kama mkwamo unatoka rohoni, hauhusiani kabisa na fikra na uchambuzi uliofanya, yaani kila kitu kiko sawa kwenye fikra ila ndani yako kunakuwa na uzito, hiyo inatoka kwenye nafsi na sikiliza.

Kwa kusikiliza nafsi yako kuna wakati utakosa fursa nzuri, lakini utajiepusha na fursa nyingi mbaya kwako.

Hatua ya kuchukua;
Isikilize nafsi yako kwenye maamuzi unayofanya, yawe kweli yametoka ndani yako na siyo kusukumwa na tamaa fulani. Kama nafsi yako hairidhii kufanya kitu fulani, usikifanye, hata kama kinaonekana kuwa na manufaa.

Tafakari;
Nafsi yako huwa haisahau, inajua vitu vingi ambavyo akili yako haikumbuki tena. Hivyo inaposita kwenye kitu, ni kwa sababu kuna kumbukumbu zisizo nzuri kuhusu kitu cha aina hiyo umewahi kufanya huko nyuma. Isikilize nafsi yako.

Kocha.