Rafiki yangu mpendwa,
Aliyekufa mnenaji, muuzaji na mhamasishaji Zig Zigler amewahi kushirikisha hadithi fupi yenye funzo kubwa sana.
Hadithi inakwenda kama ifuatavyo.
Mfalme mmoja aliwakusanya watu wote wenye hekima waliokuwa kwenye himaya yake.
Akawaambia anawapa jukumu la kutengeneza falsafa kuu ya maisha, falsafa ambayo watu wa himaya yake wakiielewa na kuiishi, maisha yao yatakuwa bora sana.
Watu hao walitoka na kwenda kufanya utafiti wa kina, kusoma kila aina ya kitabu na kisha kuandika falsafa ambayo waliamini itamfaa kila mtu.
Baada ya kukamilisha kazi hiyo walirudi kwa mfalme wakiwa na vitabu 12 walivyoandika kuelezea falsafa hiyo.
Mfalme aliwapongeza kwa kazi kubwa waliyofanya, akiwaambia anaamini ni falsafa nzuri kabisa. Ila vitabu 12 ni vigumu watu kusoma vyote na kuelewa.
Hivyo aliwataka waende wakakae tena wafupishe falsafa hiyo.
Watu hao waliondoka na kwenda kufanyia kazi hilo. Baada ya muda walirudi kwa mfalme wakiwa na vitabu sita. Mfalme akawaambia bado ni ndefu sana.
Wakaenda kufanyia kazi na kurudi na kitabu kimoja, akawaambia bado ni ndefu.
Wakarudi kwenda kufanyia kazi na wakarudi na ukurasa mmoja, mfalme alifurahi, ila akawaambia bado, wafupishe zaidi.
Wakaondoka na kurudi na aya moja, bado mfalme akawaambia ni ndefu.
Watu hao wakaondoka tena na kwenda kufanyia kazi hilo kwa muda, kisha wakarudi kwa mfalme wakiwa a sentensi moja tu.
Mfalme aliisoma sentensi ile, akatabasamu na kuwaambia watu wale hapa kweli mmekuja na falsafa sahihi na hii ndiyo kila mtu wa himaya yangu anapaswa kuijua na kuiishi.
Sentensi hiyo ilisomeka; HAKUNA KITU CHA BURE.

Ni sentensi fupi sana, lakini yenye maana kubwa mno, ambayo ukiielewa na kuiishi, utakuwa na maisha bora kabisa.
Matatizo mengi ambayo tunakutana nayo kwenye maisha ni matokeo ya kujaribu kwenda kinyume na falsafa hiyo.
Pale mtu unapotaka kupata kitu cha bure, ndiyo unaingia gharama kubwa mno kwenye maisha yako.
Kupenda vitu vya bure ndiyo imepelekea wengi kulaghaiwa na kutapeliwa. Kwa kuonyeshwa kuna mamna ya kupata kitu bure, wanaingia tamaa na hilo kupelekea kutapeliwa.
Kwa kupenda vitu vya bure kumefanya wengi walipe gharama kubwa bila kujua kama wanafanya hivyo. Mtu anaambiwa anapewa kitu bure, ila kinakuja na masharti ambayo ni makali kuliko angeingia gharama kupata kitu hicho.
Na wakati mwingine wewe unaweza kupata kitu bure, lakini kuna wengine wanakuwa wamekigharamia bila ya wewe kujua.
Ishi kwa falsafa hii kila siku, ukijikumbusha hakuna kitu cha bure, hivyo mtu anapokuja kwako kwa kukushawishi na bure, unaanza kuangalia wapi gharama zimejificha.
Hata pale serikali inapokuambia inatoa huduma fulani bure, hakuna bure. Unalipia kwa kodi unazotozwa, usumbufu unaopata na hata misaada yenye masharti ambayo serikali inapewa.
Kadhalika biashara yoyote inapokuambia unapata kitu bure, jua kuna gharama zimejificha ambazo huwezi kuziona kama haupo makini.
Chukua mfano wa mitandao ya kijamii, wengi wanaipenda na kuitumia kwa sababu ni bure, hulipii kutumia.
Lakini mitandao hiyo inaingiza faida kubwa sana, kwa sababu watumiaji wa mitandao hiyo ndiyo bidhaa inayouzwa.
Wakati wewe unafurahia kutumia mitandao ya kijamii bure, wenye mitandao wanafurahia kupata muda wako, umakini wako na taarifa zako kisha kuziuza kwa wale wanaozihitaji kwa mambo mbalimbali, kubwa likiwa kukutangazia na kukushawishi kwenye mambo mbalimbali.
Kama umechoka kuwa bidhaa kwenye hii mitandao ya kijamii ni wakati sasa wa kusoma kitabu cha EPUKA UTUMWA WA KIDIJITALI.
Kitabu hicho kimeeleza jinsi mitandao imekujengea uraibu ili iendelee kukutumia wewe kama bidhaa.
Ni wakati sasa wa kuvunja uraibu huo ili uweze kuwa huru.
Jipatie nakala yako ya kitabu leo ili uondoke kwenye gereza ulilowekwa bila kujijua na kuwa huru na maisha yako. Wasiliana na 0752 977 170 ili kupata kitabu hiki kizuri kinachokwenda kukufungua kwa kiwango kikubwa sana.

Jikumbushe kila wakati kwamba hakuna kitu cha bure. Hivyo unaposhawishiwa na bure, jua kuna namna unalipa bila kujua au kuna watu wanalipa bila wewe kujua.
Kwa vyovyote vile, kupenda na kukubali vitu vya bure ni kuchagua kupoteza uhuru wako.
Linda uhuru wako kwa kulipa gharama ya kila unachojihusisha nacho, kwa sababu hakuna kitu cha bure kwenye haya maisha.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.
www.somavitabu.co.tz