2502; Hiyo Pesa Itafute Hapo Ulipo Kwanza.

Fursa mpya zimekuwa haziishi na zinashawishi kweli kweli.
Maana ni vigumu sana kuikataa pesa wakati una uhitaji mkubwa wa fedha.

Hivyo zinapokuja fursa mpya, ambazo tunakua kabisa kwamba haziendani na kile tunachofanya, tukishaona kuna fedha tunaweza kupata, basi tunakimbilia kuifanya.

Mwisho wake kinachotokea ni fedha tuliyotegea kupata hatupati na tumepunguza umakini kwenye kile kikuu tunachopaswa kufanya.

Unaweza kudhani baada ya kukosa pesa tuliyotegemea tungejifunza ili wakati mwingine hilo lisijitokeze tena.
Lakini hilo halitokei, kila mara fursa mpya ikija yenye ushawishi wa pesa unanasa na kuhangaika nayo na matokeo yanayopatikana siyo makubwa sana.

Hata kama utapata kweli pesa ambayo ulishawishika kuingia kufanya bado siyo nyingi kama ambayo umeipoteza kwa kupunguza umakini wako kwenye kile kikuu unachopaswa kufanya.

Hatua ya kuchukua;
Kwa kila fursa mpya unayokutana nayo na kushawishika ni fursa nzuri kwako kwa sababu kuna pesa unayoweza kupata, usikimbilie kuifanya moja kwa moja.
Badala yake jiulize ni kiasi gani cha pesa unachoweza kupata kwenye fursa hiyo mpya.
Ukishapata kiasi hicho, jiulize unawezaje kupata kiasi hicho cha fedha kwa ziada kwenye kile unachofanya sasa.
Lengo ni upate hiyo pesa unayotaka, kwenye kile kikuu ambacho tayari unakifanya.
Na hilo linawezekana kabisa ukijiuliza maswali muhimu na kujipa majibu.
Uzuri ni ukipata njia ya kuongeza kipato kwa kile unachofanya sasa, utazidi kubobea kwenye kitu hicho zaidi na hutahangaika na mambo mengi ya tofauti.

Tafakari;
Hapo hapo ulipo, kwenye hicho hicho unachofanya bado kuna fursa nyingi ambazo hujazotumia. Kabla hujakimbilia mbali kwenye fursa za kutengeneza pesa zaidi, anzia hapo hapo ulipo.

Kocha.