#SheriaYaLeo (10/366); Kubali na Ishi uajabu wako.

Kuna namna ambavyo uko tofauti kabisa na watu wengine.
Utofauti huo umewafanya watu wakuone wewe ni mtu wa ajabu.
Uajabu wako huo umekuwa unawafanya baadhi ya watu wakuchukie, wakudharau, wakupinge na hata wakukosoe.
Kwa sababu tunapenda sana kukubalika na wengine, huwa tunakuwa tayari kuacha uajabu wetu na kufanya kile kinachokubalika na wengine.

Na hapo ndipo tunapopoteza nguvu zetu na fursa ya kufanya makubwa.
Tunapoacha uajabu wetu na kufanya yaliyozoeleka, tunaishia kuwa kawaida na hakuna makubwa tunayofanya.
Lakini kwa kukubali na kuishi uajabu ulio ndani yetu, kuna wengi tutawaudhi, lakini pia tutafanya makubwa ambayo hayajawahi kufanywa hapo kabla.

Watu wote waliofanya makubwa hapa duniani, hawakuiga yale wengine walikuwa wanafanya.
Bali walikubali na kuishi uajabu wao.
Kwa namna hiyo walipata ukosoaji na upingwaji mkubwa, lakini pia waliweza kufanya makubwa.
Walionekana ni watu wa ajabu na wakati mwingine kuchukuliwa kama wamechanganyikiwa.

Kubali na kuishi upekee, utofauti na uajabu wako, pamoja na madhaifu yake.
Tumia uajabu huo kufanya mambo ambayo hayajazoeleka.
Na hapo ndipo unaweza kufanya makubwa na kuacha alama hapa duniani.
Usifiche au kupuuza chochote cha tofauti na cha ajabu kilicho ndani yako kwa sababu tu watu hawakielewi.
Hakuna aliyewahi kufanya makubwa ambaye mwanzo alieleweka.

Sheria ya leo; Mara zote kaa kwenye yale yanayokufanya wa tofauti, wa ajabu na usiyefaa. Hicho ndiyo chanzo cha nguvu zako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma