2509; Kwa nini hupendi unachofanya?
Kutokupenda kazi au biashara unayofanya ni kikwazo kikubwa cha mafanikio yako.
Huwezi kufanikiwa kwenye kitu ambacho hukipendi, hata kama kinalipa kiasi gani.
Huenda wewe ni mmoja wa wale ambao wanafanya wasichopenda, leo nataka upate jawabu hapa ili kuchukua hatua sahihi.
Mahali pa kuanzia ni kujua kwa nini hupendi kile unachofanya.
Haitokei tu, lazima kuna sababu inayopelekea hilo.
Inawezekana ni mawazo yako kuwa kwenye kitu tofauti na kile unachofanya. Yaani unafanya kitu hiki, lakini mawazo yako yapo kwenye kitu kingine kabisa.
Hili utalitatua kwa kujenga uwepo wa kiakili kwenye kile unachofanya.
Kwa kuhakikisha mawazo yako yote yapo kwenye kile unachofanya, hata kama siyo cha ndoto yako.
Kwa kuweka mawazo na umakini wako wote kwenye kitu, utakifanya vizuri na hivyo kukipenda.
Inawezekana huna udhibiti wa kutosha kwenye kile unachofanya. Mambo mengi unafanya kwa kulazimishwa na siyo kwa kuchagua mwenyewe.
Hili unaweza kulitatua kwa kutafuta eneo unaloweza kuwa na udhibiti nalo kwenye hicho unachofanya, hata kama ni dogo kiasi gani.
Inawezekana ni watu unaofanya nao ndiyo wamekuwa wanakukwamisha na kufanya uone ugumu kwenye kufanya.
Hili utaondokana nalo kwa kuacha kuyaangalia madhaifu ya watu na kuangalia uimara wao.
Au pale inapowezekana, kuachana na watu hao, hasa wanapokuwa mzigo mkubwa kwako.
Na pia inawezekana unakosa ubobezi kwenye hicho unachofanya. Unashindwa kukifanya vizuri na hilo kupelekea uzalishe matokeo yasiyo mazuri, kitu kinachokukwamisha zaidi.
Hili unalitatua kwa kujenga ubobezi kwenye kile unachofanya, kwa kuhakikisha unakifanya kwa ubora wa hali ya juu kabisa.
Hatua ya kuchukua;
Mara nyingi unakuwa hupendi unachofanya kwa sababu ya ubinafsi wako mwenyewe. Unajiangalia zaidi wewe unapata nini kuliko kuangalia wengine pia wananufaikaje. Hakuna unachofanya kisiwe na manufaa kwa yeyote, angalia watu gani wananufaika na unachofanya na wananufaikaje na hilo litakupa sababu ya kukipenda.
Tafakari;
Chochote unachoruhusu mikono yako kufanya, kifanye kwa upendo na kwa ubora wa juu kabisa. Na kama hilo haliwezekani basi bora uache kabisa kufanya. Maana ya kufanya ni mengi, usijifunge kwenye kitu ambacho huwezi kufanikiwa kwa kuwa hukipendi.
Kocha.