2510; Kwa nini hubadiliki?

Kuna nukuu moja maarufu sana inayosema; miaka mitano ijayo utakuwa mtu yule yule uliye sasa isipokuwa kwa watu utakaokutana nao na vitabu utakavyosoma.

Ni kauli rahisi lakini yenye funzo na maana kubwa sana.
Kwamba mafanikio yetu kwenye maisha yanatokana na mabadiliko yanayotokea kwenye maisha yetu.
Mabadiliko hayo yanachochewa na vitu viwili vikubwa; watu na vitabu.

Hivyo kama hufanikiwi kupiga hatua kubwa ni kwa sababu huna mabadiliko yoyote kwenye maisha yako. Na huna mabadiliko kwa sababu husomi vitabu na hukutani na watu wapya.

Kukutana na watu wapya ni pale unapopata fursa ya kujenga mahusiano na kufanya kazi na watu tofauti na wale uliowazoea. Hilo linakupa nafasi ya kujifunza vitu tofauti kutoka kwa watu hao.
Hilo pia linaweza kutokana na kusafiri maeneo mbalimbali na kujifunza vitu ambavyo hukuwa unavijua.

Kusoma vitabu hilo liko wazi, kupitia usomaji wa vitabu unapata maarifa mapya na yanayofungua zaidi mtazamo ulionao.
Kusoma vitabu ni mbadala wa kusafiri au kukutana na watu wapya.

Hatua ya kuchukua;
Kila siku tafuta fursa ya kujifunza kitu kipya kupitia watu unaokutana nao na vitabu unavyosoma.
Usikubali siku iishe hujajifunza chochote kipya na kubadilika.
Maana utakuwa umechagua kutokufanikiwa.

Tafakari;
Kama hakuna kipya kinachoingia ndani yako, hakuna cha tofauti unachoweza kufanya. Kama hakuna cha tofauti unachofanya, huwezi kufanikiwa.

Kocha.