2511; Hawajui unachojua wewe.

Watu wanaweza kukushangaa kwa yake unayofanya.
Wanaweza kwenda mbali zaidi na kukukosoa au kukupinga.
Lakini wengi wanafanya hivyo bila kujua mengi ambayo wewe unayajua.

Kwa kuwa wana taarifa chache na za juu juu tu, ni rahisi kwao kuona unachofanya siyo sawa.
Lakini kama wakipata taarifa za ndani na za kina, watajionea wenyewe kwamba wanachofikiria wap pia siyo sawa.

Kwa bahati mbaya sana tunaishi kwenye jamii na zama ambazo watu wapo haraka sana kutoa maoni yao kwenye kila jambo. Mitandao ya kijamii imerahisisha hilo la kila mtu kutoa maoni.
Lakini mengi ni maoni ambayo yanatokana na taarifa ambazo hazijakamilika.

Hatua ya kuchukua;
Kama unataka mtu akushauri jambo, mweleze kwa kina ajue kila unachojua na unachohisi kwenye jambo husika. Hapo yeye mwenyewe ataona jinsi ambavyo kufanya maamuzi ni kugumu.
Usikimbilie kushauri watu au kutoa maoni yako kama huna taarifa za kutosha juu ya jambo husika.

Tafakari ya leo;
Ni rahisi kutoa maoni na ushauri kwa kuwa na taarifa chache na za juu juu kuhusu jambo. Lakini unapokuwa na taarifa za ndani na za kina, maamuzi yanakuwa magumu kufikia. Jua hili ili uweze kupembua ushauri na maoni unayotoa au kupokea kutoka kwa wengine.

Kocha.