#SheriaYaLeo (15/366); Acha Kusudi Likuongoze.
Kitu muhimu ambacho watu wengi wanakikosa kwenye zama tunazoishi sasa ni kusudi kubwa la maisha yao.
Kipindi cha nyuma watu walipewa kusudi la maisha na dini au jamii zao.
Kwa sababu kipindi hicho dini na jamii zilikuwa na nguvu kubwa ya kuwaamulia watu maisha yao.
Lakini sasa tunaishi kwenye zama ambazo dini na jamii havina tena nguvu ya kumwamulia mtu kuhusu maisha.
Na hapo ndipo changamoto kubwa inapoanzia, kwa sababu watu wanajikuta wakihangaika na mambo mengi yasiyo na tija kwao.
Sisi binadamu ni tofauti na wanyama wengine kwa sababu tuna uwezo wa kutengeneza dunia yetu wenyewe.
Hatuendeshi maisha kwa hisia na misukumo ya mwili pekee, bali tuna uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi muhimu.
Lakini mtu asipokuwa na kusudi kubwa linaloongoza maisha yake, anaishia kufanya maamuzi ya hovyo.
Mtu anashindwa kutumia muda na nguvu zake vizuri.
Hili linapelekea hali ya utupu kwenye maisha ya mtu.
Licha ya kufanya mengi, lakini bado mtu anaona hakuna alichofanya, kwa sababu hajatimiza kusudi ambalo ni kubwa kuliko yeye.
Kujua kwamba umeletwa hapa duniani kwa jukumu maalumu, ukiwa na kusudi kubwa unalopaswa kulikamilisha ndiyo njia bora ya kuyaishi maisha yako na kufanya makubwa.
Kulijua kusudi la maisha yako ni wajiby muhimu unaopaswa kuufanyia kazi.
Hupaswi kuona ni kitu cha ajabu au ubinafsi kufanya hivyo.
Hiyo ndiyo namna pekee ya kuweza kuacha alama kubwa hapa duniani.
Mageuzi na maendeleo makubwa ambayo binadamu tumeweza kuyaleta hapa duniani, ni matokeo ya watu kuweza kujua na kuliishi kusudi kubwa la maisha yao bila kujali wengine wanasema au kufanya nini.
Sheria ya leo; Fikiria nyakati ambazo ulikuwa na muunganiko mkubwa na kile ulichokuwa unafanya. Fikiria raha na ridhiko kubwa ulilolipata kwenye kufanya kitu hicho. Kwenye vitu hivyo ndipo penye kusudi la maisha yako. Acha kusudi likuongoze na utaweza kufanya makubwa.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma