2512; Kuna wengine pia.

Ukiona mende mmoja ndani ya nyumba, jua kabisa mende huyo hayupo peke yake. Kuna mende wengine pia, hata kama huwaoni, wewe jua wapo.
Unapaswa kutumia fursa uliyoipata ya kumuona mende mmoja kuhakikisha unaondoa mende wengine wot.
Usiue mende mmoja uliyemuona na kudhani umemaliza tatizo.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye maisha, kazi na biashara. Unapokutana na mtu wa aina fulani, jua hayupo peke yake, kuna wengine pia.
Wajibu wako ni kutumia fursa ya huyo uliyekutana naye kutatua kwa wengi pia.

Kama kuna mteja mmoja anasema vitu vyako wewe unauza ghali kuliko wengine, hata kama unajua siyo kweli usipuuze hilo.
Kuna mtazamo ambao anao, ambao wapo wengine pia wanao kuhusu biashara yako.
Badala ya kumchukia huyo aliyekuambia hilo, mtumie yeye kama fursa ya kuweza kubadili mtazamo huo ambao wapo wengine walionao.

Kuna mitazamo ya tofauti kuhusu wewe binafsi na yale unayofanya ambayo watu wamejijengea. Unaweza usiijue yote, lakini kwa bahati nzuri sana kuna wakati utapata fursa ya mtu mmoja kuonyesha mtazamo fulani kwako.
Wajibu wako ni kutumia hiyo fursa kubadili mtazamo huo kwa walio wengi pia.

Kadhalika hata kwa upande wa mazuri, kama umepata mteja au mfanyakazi mzuri sana, ambaye anafanya uone mambo ni rahisi na yanawezekana, jua hayupo mwenyewe. Kuna wengine kama yeye, hivyo wajibu wako ni kujua wapi wanapatikana ili uweze kuwafikia.

Hatua ya kuchukua;
Kwa kila kitu cha tofauti unachoona au kukutana nacho, jua hakipo peke yake. Kuna vingine kama hivyo ambavyo havionekani. Tumia fursa ya kile ulichoona kuweza kuboresha hata yale yasiyoonekana.

Tafakari;
Maisha yana namna ya kuleta fursa nzuri kwetu kwa kificho, usipokuwa makini unaweza kuzipoteza. Chukulia kila kitu kama fursa na utaona jinsi mambo mengi unayokutana nayo yalivyo na manufaa.

Kocha.