#SheriaYaLeo (16/366); Hakuna Wito Bora Zaidi Ya Mwingine.
Tambua kwamba mchango wako kwenye jamii unaweza kuja kwa namna tofauti tofauti.
Siyo lazima uwe mjasiriamali mkubwa, kiongozi mkubwa au mvumbuzi ndiyo uweze kuleta mchango mkubwa kwenye jamii.
Unaweza kufanya makubwa ukiwa peke yako au ukiwa ndani ya taasisi kubwa.
Muhimu ni kile unachofanya kitoke ndani yako kweli na ukitumie kuleta matokeo ya tofauti kwa wengine.
Mchango wako unaweza kuwa ni kupitia kazi ya mikono yako, ambapo unaacha alama kubwa kwenye kila unachofanya.
Mchango wako unaweza kuwa ni jinsi unavyolea familia yako, kwa namna bora kabisa na ya kipekee, ambayo dunia haijawahi kuona.
Usidanganyike kwamba mpaka ufanye kitu cha aina fulani ndiyo utakuwa na wito au kusudi sahihi.
Chochote kinachotoka ndani yako kweli ndiyo wito na kusudi sahihi kwako.
Wajibu wako mkubwa ni kuhakikisha chochote unachokifanya, unakifanya kwa upekee na utofauti mkubwa, kwa namna ambayo dunia haijawahi kuona.
Kwa kufanya hivyo, utaweza kuwa wa tofauti kabisa kwenye hii dunia ambayo wengi wanafanya mambo yanayoweza kufanywa na wengine.
Ni utofauti huo ndiyo utakaokuwezesha kuwa na uhuru na mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Sheria ya leo; Hakuna wito au kusudi ambalo ni bora zaidi ya mengine. Muhimu ni wito au kusudi lako litoke ndani yako kweli na uwe na msukumo mkubwa ndani yako wa kufanya kwa tofauti na upekee huku ukiendelea kujifunza na kuboresha kadiri unavyoendelea kwenda.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma