#SheriaYaLeo (18/366); Acha Kutaka Kumfurahisha Kila Mtu.

Utalipa gharama kubwa sana kwa kutaka kumfurahisha kila mtu na kuonekana kujali kuliko kuyaishi maisha yako halisi na kuonyesha kivuli chako.

Kuyaishi maisha yako;
Kwanza kabisa unapaswa kuheshimu maoni yako kuliko ya wengine, hasa inapokuja kwenye eneo lako la ubobezi, eneo ambalo umechagua kuzama. Amini uwezo wako mkubwa na mawazo ya kipekee unayokuwa nayo kwenye eneo hilo.

Pili jenga tabia ya kuwa na msimamo kwenye mambo yako na kuacha kuvunja msimamo yako ili kuwaridhisha wengine. Fanya hili kwenye kila fursa ya kulitekeleza inayojitokeza.

Tatu acha kujali sana wengine wanakufikiriaje. Utapata uhuru mkubwa kwa kuvuka hili.

Nne tambua kuna nyakati utapaswa kuwaudhi na hata kuwaumiza watu wanaoziba njia yako, watu wenye nia mbaya ya kukuzuia usifike unakotaka. Tumia nyakati kama hizo kuwaonyesha watu uhalisia wako, ili wajue hutanii kwenye kile unachotaka.

Tano jisikie huru kuonyesha ujinga na unafiki wa watu wengine wanaojaribu kuwa kikwazo kwako.

Sita kataa mazoea ambayo wengine wanayafuata kwenye yale wanayofanya.

Huwezi kupata kile unachotaka kama haupo tayari kuwa wewe pamoja na madhaifu uliyonayo.
Huwezi kuwa wewe kama unataka kumfurahisha na kumridhisha kila mtu.

Sheria ya leo; Tambua kwamba nguvu yako ipo kwenye kusimamia upekee wako hata kama itabidi kuwaudhi wengine katika kufanya hivyo. Ujue upande wako halisi ambao unaweza usipende sana kuuonyesha kwa wengine.

#NidhamhUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma