2520; Mahali unapojificha.

Kila mmoja kuna mahali huwa anajificha inapokuja kwenye uhitaji wa kufanya makubwa ili kufanikiwa.

Kufanya hayo makubwa ni kugumu na pia matokeo siyo ya uhakika sana.
Wakati huo sisi binadamu huwa ni wavivu na tunapenda vitu vya uhakika.

Hivyo tunapokabiliwa na kitu kikubwa cha kufanya mbele yetu, huwa tunakimbilia kujificha.

Kwa bahati mbaya sana, siyo rahisi kujua kama utajificha, kwa sababu hujiambii kama unajificha.
Unachojiambia ni sababu na visingizio mbalimbali vya kwa nini huwezi kufanya unachopaswa kufanya.

Sababu na visingizio hivyo vinaweza kuonekana ni sahihi kabisa.
Lakini mwisho wa siku iko wazi kwamba hujafanya unachopaswa kufanya na hivyo hujapata matokeo sahihi.

Utajiambia hujawa tayari, hali siyo nzuri, hakuna watu sahihi na mengine mengi. Lakini yote hayo ni kujificha tu.

Kwenye safari ya mafanikio ni unafanya au hufanyi, mengine yote ni kujificha tu.

Hatua ya kuchukua;
Jikamate wakati unajificha. Kama kuna kitu unapaswa kufanya na hukifanyi, haijalishi unajipa sababu gani, jikumbushe tu kwamba unajificha. Ukijikamata mwenyewe ni rahisi kujisukuma kufanya kuliko kuendelea kujidanganya.

Tafakari;
Chagua kufanya au chagua kutokufanya, usipoteze muda kueleza sababu na visingizio, ni njia za kujificha ambazo hazina msaada kwa yeyote.

Kocha.