#SheriaYaLeo (24/366); Unganisha yale unayopendelea.

Wakati mwingine kusudi na wito wako hautokani na kitu kimoja, bali unatokana na kuunganisha vitu ambavyo unapendelea kufanya.
Kwa kujua vitu hivyo na kuviunganisha pamoja unaweza kutengeneza kitu cha kipekee kabisa kwako.

Kama bado ni kijana na ndiyo unaianza safari yako, unapaswa kujaribu mambo mbalimbali yanayokuvutia.
Kwa mfano kama unapenda kuandika, unapaswa kujaribu mitindo mbalimbali ya uandishi mpaka utakapokutana na mtindo unaoendana na wewe vizuri zaidi.

Kama ni mzee tayari una uzoefu kwenye mengi uliyopitia. Chukua ujuzi wote uliojijengea katika safari yako na uunganishe kwa namna ambayo utakuwa bora kabisa kwako.

Wote waliofanya makubwa na kufanikiwa sana, waliunganisha maeneo waliyoyapenda na kuzalisha kitu cha kipekee kabisa.
Mfano Steve Jobs aliunganisha teknolojia na ubunifu na kuweza kuja na vitu vipya na vya kipekee kabisa kama simu janja.

Sheria ya leo; Tambua kwamba wito wako unaweza kutokana na kuunganisha tasnia mbalimbali unazozipendelea. Usijifunge mapema, kuwa tayari kujaribu mengi unayopendelea na utaona fursa za kuyaunganisha na kupata kitu cha kipekee.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#Ubunifu