2522; Kama unajua sana, mbona matokeo hayaonyeshi huo ujuaji?

Kwenye safari ya mafanikio, hakuna sumu kubwa kama ujuaji.
Sumu hii huanza pale mtu anapoona yale anayofundishwa tayari anayajua.

Kwa sababu maarifa na siri za mafanikio ni zile zile, wengi hufika mahali na kuona wameshajua kila kitu, hakuna tena kitu kipya.

Lakini unapoyaangalia maisha yao kwa uhalisia, hayaakisi kile ambacho wanasema wanajua.
Watakuambia tayari wanajua kila kitu kuhusu mafanikio, lakini maisha yao hayana mafanikio, wala hawapo kwenye safari sahihi ya mafanikio.

Wengine hujifunza, lakini inapofika kwenye kuchukua hatua, kufanyia kazi yale waliyojifunza wanaona kama ni utoto, wanaona hayo yapo chini yao sana, hawawezi kuhangaika nayo.
Lakini unaporudi kuyaangalia maisha yao, hayaendani na hiyo hadhi wanayojipa.

Mafanikio siyo maneno, bali ni matokeo na kama ujuaji wako haujakupa mafanikio basi huo siyo ujuaji sahihi. Kwa kifupi ni huna unachojua au huenda hicho unachosema unajua ndiyo kikwazo cha wewe kufanikiwa.

Hatua ya kuchukua;
Kama unataka kufanikiwa kweli na kudumu kwenye mafanikio yako, basi kila wakati unapaswa kuwa tayari kujifunza na kuyafanyia kazi yale unayojifunza.
Hata kama unaona ni mambo unayoyajua na hakuna jipya, kaa chini na ujifunze. Kwa kurudia kujifunza unayodhani unajua, kuna mengi mapya utakayoondoka nayo.
Kwa kufanyia kazi haraka yale unayojifunza unayafanya kuwa sehemu ya maisha yako.
Kujifunza na kuchukua hatua ni kitu ambacho hakina ukomo kwenye safari ya mafanikio.

Tafakari;
Kama unasema tayari unajua lakini hujafanikiwa, basi jua hujui.
Kama unasema tayari unajua na umeshafanikiwa, kuna hatari ya anguko mbele yako.
Mafanikio na ujuaji havijawahi kwenda pamoja.

Kocha.