#SheriaYaLeo (26/366); Epuka Nguvu Zinazokuzuia Usifikie Ubobezi.

Una nguvu kubwa ndani yako ambayo inakufanya wa tofauti na wa kipekee, nguvu hiyo ndiyo imebeba wito na kusudi lako.

Lakini pia kuna nguvu kubwa za nje ambazo zinaipinga nguvu hiyo ya ndani na kukuzuia usiweze kuitumia ili kujitofautisha na kufanya makubwa.

Nguvu hizo zinatokana na msukumo wa kijamii wa kutaka uwe kama wengine.
Jamii huwa haitaki uwe wewe na kuwa huru kufanya mambo yake.
Badala yake inataka uwe kama wengine na ufuate mkumbo.

Wazazi pia wanaweza kuwa sehemu ha nguvu hiyo, wanawaze kukulazimisha ufanye kazi ya aina fulani kwa sababu hawataki usumbuke au kuteseka.

Nguvu hizo zinazokuzuia usifikie ubobezi zinapokuwa kubwa, zinakuondoa kabisa kwenye upekee wako na kukufanya kama wengine.
Unaishia kuwa kama wengine, unashindana nao na kuishia kuwa wa kawaida.

Hilo linakuweka kwenye njia hatari kwa sababu unachochagua kufanya kinakuwa hakijatoka ndani yako kweli.
Hufurahii kile unachofanya na hivyo kulazimika kutafuta raha nje ya kile unachofanya.
Hilo linapelekea usiwe na umakini wa kutosha kwenye kazi yako na hivyo kuzikosa fursa nzuri na za kipekee zinazokuwa zinajitokeza kwenye kile unachofanya.

Unashindwa kufanya maamuzi muhimu wewe mwenyewe na kuishia kufuata mkumbo na kusikiliza wengine.
Unapokwenda hivyo kwa muda mrefu unajisahau kabisa na kutoweza kujitofautisha na wengine.
Kwa gharama zozote zile unapaswa kuepuka nguvu hizo zinazokinzana na upekee wako.

Sheria ya leo; Mchakato wa kufuata wito wa maisha yako mpaka kufikia ubobezi unaweza kuanza kwenye hatua yoyote ya maisha yako. Nguvu kubwa ya kuikamilisha safari hiyo tayari ipo ndani yako ikisubiri kutumika. Unaweza kutumia nguvu hiyo kubwa ya ndani kama tu utaweza kutuliza nguvu za nje zinazoipinga.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#Ubunifu