#SheriaYaLeo (27/366); Siri Kuu Ya Mafanikio.
Tangu enzi na enzi, watu wamekuwa wanatafuta njia za mkato na kanuni zahisi za kufanikiwa.
Lakini mwisho wa siku wanaishia kupotea, kwa sababu hivi ni vitu ambavyo havipo kabisa.
Wakati unahangaika kutafuta njia hizo za mkato zisizokuwepo, unapuuza nguvu kubwa ambayo tayari ipo ndani yako.
Nguvu hiyo ina matokeo halisi kwa sababu imekuwa inatumiwa miaka kwa miaka na wale ambao wameweza kufanya uvumbuzi mkubwa hapa duniani.
Kila maendeleo unayoyaona hapa duniani, ni matokeo ya watu kutumia nguvu hiyo kubwa iliyo ndani yao.
Wale wanaoitumia nguvu hiyo wanapata muunganiko na nguvu kubwa inayouendesha ulimwengu na kuweza kuitumia kufanya makubwa.
Kwa miaka mingi, watu wamejenga uzio kuzunguka ubobezi.
Wameufanya uonekane ni kitu wanachoweza kufikia watu wachache, wale wenye akili na uwezo mkubwa.
Wamefanya watu wa kawaida waone ubobezi ni kwa wachache waliozaliwa na vipaji fulani au kwenye familia za aina fulani.
Lakini huo wote ni uongo.
Siri kuu ya ubobezi na mafanikio makubwa ni hii; unamiliki ubongo wenye uwezo mkubwa sana. Ubongo huo umetengenezwa kwa mageuzi ya zaidi ya miama milioni sita ya maendeleo. Ubongo huo pamoja na uwezo wake mkubwa vipo ndani yako, ni wewe kuweza kuvifikia na kuvitumia kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Chochote unachotaka kinaanzia kwenye akili yako, hiyo ndiyo nguvu kubwa na siri kuu ya mafanikio.
Sheria Ya Leo; Fanyia kazi kutengeneza aina ya akili unayoitaka. Kuachilia uwezo mkubwa wa akili yako ndiyo njia pekee ya kufikia ubobezi, kufanya makubwa na kupata mafanikio makubwa.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#Ubunifu