2527; Kila suluhisho ni tatizo.

Kwenye maisha huwa tunapitia matatizo na changamoto mbalimbali.
Hilo hutusukuna kutafuta suluhisho ili maisha yetu yaweze kwenda vile tunavyotaka.

Tunachosahau au ambacho tunakuwa hatujui wakati tunatafuta suluhisho ni kwamba kila suluhisho huwa lina tatizo ndani yake.
Ndiyo ni suluhisho la tatizo ambalo unalo, lakini ndani ya hilo suluhisho kuna tatizo jingine.

Wengi tunakosea pale tunapodhani suluhisho tunalopata ni safi, halina matatizo yoyote. Na hapo ndipo tunapotengeneza matatizo makubwa zaidi ya yale tunayojaribu kutatua.

Ndiyo una tatizo la fedha na unaona kukopa ni suluhisho. Lakini jua ndani ya mkopo kuna riba, inayokutaka ulipe kiasi kikubwa kuliko unachopewa.

Ndiyo umechoka au umevirugwa na unataka kujiburudisha kidogo kwa kilevi. Lakini tambua kilevi kinapumbaza akili zako kwa muda na kuuchosha zaidi mwili wako.

Ndiyo kuna watu wamekukosea na unastahili huwaadhibu. Lakini tambua adhabu unayowapa inaweza kujenga kinyongo ndani yao na wakataka kulipiza kisasi kwa namna fulani.

Hakuna suluhishi lisilokuwa na matatizo. Hivyo katika kufanya maamuzi, msingi mkuu ni kuchagua suluhisho ambalo matatizo yake unaweza kuyamudu.

Hatua za kuchukua;
Ni changamoto zipi unazosuluhisha sasa ambazo hujaangalia matatizo yanayotokana na suluhisho unalopata? Anza sasa kuangalia kwa kina kila suluhisho na kujua ni matatizo gani yako ndani yake.

Tafakari;
Kadiri inavyokuwa rahisi kupata suluhisho na kitu, ndivyo suluhisho hilo linakuwa na matatizo makubwa zaidi. Usikubali kufikia suluhisho lolote kabla ya kujua matatizo yake ns kuona kama unaweza kuyamudu.

Kocha.