2528; Kutaka vingi kwa pamoja.
Hadithi tulizokuwa tunajifunza utotoni zilikuwa na masomo makubwa sana kuhusu maisha.
Lakini kwa bahati mbaya sana tumekuwa hatuzipi uzito na hivyo kufanya makosa ambayo hadithi hizo zilikuwa zinatuasa tuyaepuke.
Chukua hadithi ya sungura kualikwa kwenye sherehe mbili.
Kwa ulafi wake akapanga asikose vyote.
Hivyo akawa anaenda huku na huku, lengo apate chakula kwenye sherehe zote.
Kwenye sherehe moja anaona chakula bado, anaamua kutoka kwenda kwenye sherehe nyingine. Huko anakuta wamemaliza kula.
Anarudi kwenye sherehe ya awali anakuta nako pia wamemaliza kula.
Masikini sungura, kwa kutaka kula kwenye sherehe zote amekosa chakula kwenye sherehe zote. Kama angeacha tamaa na kuchagua kukaa kwenye sherehe moja muda wote, angekula kwenye sherehe moja, ambayo ni bora kuliko kukosa chakuka kwenye sherehe zote mbili.
Hiyo hadithi haimhusu sungura na wala haihusu chakula. Ni hadithi inayokuhusu wewe na yale unayofanya.
Ni hadithi inayoonyesha madhara ya kutokufanya maamuzi ya kuchagua kitu kimoja na kukomaa nacho. Badala yake unahangaika na vitu vingi kwa mategemeo ya kupata kwenye vyote.
Muda wako, nguvu zako na umakini wako ni rasilimali zenye ukomo mkubwa kwenye maisha yako.
Unapozitawanya rasilimali hizo kwenye mambo mengi, unaishia kutokupata matokeo mazuri kwenye yote unayohangaika nayo.
Lakini unapowekeza rasilimali hizo kwenye mambo machache, unajiweka kwenye nafasi ya kuweza kupata matokeo mazuri.
Hatua ya kuchukua;
Jitathmini kuona ni mambo mangapi makubwa unayofanyia kazi kwa wakati mmoja. Kama yanazidi matatu umejitawanya sana na hutaweza kupata matokeo mazuri kwenye lolote. Punguza mambo makubwa unayofanyia kazi kwa wakati mmoja, ili uweze kuweka rasilimali zako maeneo sahihi na zilete matokeo bora.
Tafakari;
Kuhangaika na mambo mengi ni dalili ya kutokujiamini na kufanya maamuzi ya kuchagua mambo machache. Jiamini, chagua mambo machache na yape umakini mkubwa, itakulipa kuliko kuhangaika na mambo mengi.
Kocha.