#SheriaYaLeo (32/366); Jifunze kwa kufanya.
Ulipokuwa mdogo, wazazi na jamii ilikufundisha mambo mengi kuhusu maisha kupitia maelekezo na mifano.
Ulipoenda shule ukafundishwa mambo mengine mengi kuhusu kazi na biashara kupitia maelekezo na mifano.
Unapoingia kwenye dunia ya uhalisia, katika kuyaishi maisha na kufanya kazi au biashara, ndiyo unagundua yale uliyojifunza bado hayatoshi.
Unagundua unahitaji kujifunza tena, lakini safari hii siyo kwa kusoma, kuelekezwa au kupewa mifano, bali kwa kufanya kwa uhalisia.
Unajifunza kwa kina na kwa haraka zaidi pale unapofanya kuliko unavyoweza kujifunza kwa njia nyingine.
Lakini kwa bahati mbaya sana huna uzoefu na wala hujui yapi muhimu zaidi ya kujifunza.
Na hapo ndipo unapohitaji kutafuta mtu au watu ambao utakuwa chini yao na kujifunza kwa vitendo.
Hapa unahitaji kuwa mwanagenzi, kwa kutafuta waliobobea kwenye kile unachotaka kubobea na kufanya kazi chini yao.
Wabobezi hao watakufundisha kwa vitendo yale yote unayopaswa kujua.
Unapokuwa chini ya wabobezi hao unapaswa kuwa mnyenyekevu, kujifunza na kutii sheria na kanuni zilizopo kwenye eneo hilo.
Ni mpaka pale unapokuwa umezibobea ndiyo unawesa kuzivunja au kuziboresha zaidi.
Kujifunza kwa kufanya kuna nguvu na matokeo makubwa kama utachagua watu sahihi wa kujifunza chini yao na kuweka umakini mkubwa kwenye kile unachofanya.
Sheria ya leo; Kujifunza jinsi ya kujifunza ndiyo ujuzi muhimu sana ambao ukiubobea hakuna kitakachokushinda. Kwa sababu maisha yote ni kujifunza, unapokuwa vizuri kwenye kujifunza, hasa kwa kufanya, hakuna kinachokushinda kubobea.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu