2535; Usichoweza Kuona.

Pamoja na kwamba una uoni kamili, kuna vitu ambavyo huwezi kuviona.
Kuna upofu ambao kila mmoja wetu huwa anao.

Kuna mambo ambayo yanakuwa wazi kabisa kwa wengine, yanaonekana vizuri kabisa, lakini kwako ni giza tupu.
Watu wanaweza kudhani unapuuza, kumbe kwako ni upofu kabisa.

Ukiwa chini, upofu wako hauna madhara makubwa, kwani haupo kwenye hatua za hatari ambazo zinaweza kuwa na madhara kutokana na upofu huo.

Lakini unapokuwa kwenye nafasi za juu, upofu wako unakuwa hatari kubwa kwako, kwani madhara yake ni makubwa.
Maamuzi unayoyafanya ukiwa na upofu huo yanaweza kuwa na athari mbaya kwako na kwa wengine.

Kwa bahari mbaya sana, kadiri unavyopanda juu na kuwa na mamlaka makubwa, ndivyo unavyopoteza nafasi ya kutambua upofu wako na kuuzuia usiwe na madhara kwako.

Unazungukwa na watu wengi ambao hawapo tayari kukuambia ukweli, badala yake wanakuambia yale unayotaka kusikia.
Hata kama unakosea wazi kabisa, huku ukiwa hujui kama unakosea, hawatakua na uthubutu wa kukuambia unakosea.

Na hapo ndipo unapoelekea kwenye anguko kubwa.
Hivyo ndivyo wengi wanavyoanguka baada ya kufika ngazi za juu. Wanaangushwa na upofu wao wenyewe kwa sababu hakuna aliye tayari kuwaambia ukweli.

Hatua ya kuchukua;
Wafanye watu wawe huru kukuambia pale unapokosea. Hata kama umefika hatua za juu kiasi gani, toa fursa hiyo ya watu kukueleza makosa yako. Kuna maeneo ambayo huyaoni kutokana na upofu wako, hayo ndiyo una hatari ya kufanya makosa makubwa. Kama hakuna wanaokuambia makosa hayo yatakuangusha.
Kama wengi wanahofia kukueleza ukweli, chagua wachache ambao utawapa jukumu la kukagua makosa kwenye kila unachofanya.
Kuwa na mtu ambaye atakueleza ukweli kama ulivyo bila ya kuuficha.

Tafakari;
Kadiri unavyokwenda juu, ndivyo unavyopoteza nafasi ya kuujua uhalisia. Kwani unazungukwa na watu wengi wanaotaka kukupa habari njema za kukufurahisha kuliko habari za ukweli zinazoweza kukuumiza.
Zuia hili kwenye safari yako ya mafanikio ili lisije kuwa anguko kwako.

Kocha.