2539; Kujiridhisha kwa kujidanganya.

Mambo mengi yanayotukwamisha na kutuangusha huwa hayatokei kwa kushtukiza.
Bali yanakuwa na visababishi vinavyojulikana na ambavyo vipo wazi kabisa.

Lakini mtu unachagua kutokuona visababishi hivyo, kwa sababu ukweli unaumiza.
Hivyo unachagua kujiridhisha kwa kujifanganya.

Ni pale unapojiambia utafanya kitu kesho au baadaye. Ukweli ni huna muda wa kufanya kitu hicho, au siyo muhimu sana kwako kufanya.
Lakini hutaki kujiambia ukweli huo, hivyo unajidanganya ili tu ujiridhishe.
Ndiyo maana hiyo baadaye au kesho huwa haifikagi.
Kama huwezi kufanya kitu kwa muda uliopanga au unaohitajika kufanya, ni nadra sana ukaweza kukifanya kwenye muda mwingine.

Ni pale unapojiambia utambadilisha mtu ili muweze kwenda pamoja. Umeona wazi kuna tabia zake ambazo zitakuwa kikwazo, lakini unajiambia utambadilisha ili asiwe kikwazo.
Unajua nini kinachokuja kutokea, ni vigumu sana kumbadilisha mtu yeyote yule. Na tabia ambazo uliamini utazidhibiti, zinaishia kuwa kikwazo kwako.

Ukweli unaweza kuukimbia kwa muda, lakini huwezi kuupoteza, utaishia tu kuja kukukamata, tena kwenye wakati ambao ni mgumu zaidi kwako.

Hatua ya kuchukua;
Kwenye kila jambo, ukabili ukweli jinsi ulivyo na usitafute njia za kujiridhisha na kujifariji. Ujue ukweli na ufanyie kazi kama ulivyo. Ndiyo ukweli unaumiza, lakini unakuweka huru kuliko mengine yote.

Tafakari;
Kuna mambo machache sana ambayo hutokea kwa kushangaza kwenye maisha yetu. Ila mengi yana viashiria vingi vinavyoanza kuonekana mapema. Ukiwa mtu wa kuutafuta na kuukabili ukweli, hutajikuta kwenye hali za kushangazwa na yanayotokea.

Kocha.