#SheriaYaLeo (44/366); Jinsi ya kujifunza haraka na kwa kina.

Unapoingia kwenye mazingira yoyote mapya, wajibu wako ni kujifunza mambo mengi iwezekanavyo.
Ili kufanikisha hilo, unapaswa kurudi kwenye hali ya utoto, kwa kuona kwamba watu wengine wanajua kuliko wewe na unategemea kujifunza kwao ili na wewe uweze kubobea.

Unapaswa kuweka pembeni yale yote unayodhani unajua na kuwa mnyenyekevu na tayari kujifunza kutoka kwa kila mtu.
Unaondokana na kila aina ya hofu ya wengine watakuchukuliaje, wewe unachotaka ni kujifunza mengi na kwa kina zaidi.

Unapaswa kuwa na udadisi mkubwa, kuhoji na kufuatilia kwa kina kila kinachoendelea.
Hujiambii tayari unajua hata kama ni kitu unachojua, badala yake unakuwa tayari kujifunza kama vile hujui, hata kama ni kitu kinachojirudia rudia.

Kwa kujiweka kwenye hali hiyo ya utoto ya kujichukulia hujui na kuwa na udadisi, akili yako itafunguka sana na utakuwa na njaa kubwa ya kujifunza.
Hali hii ni ya muda tu, unajiweka kwenye utegemezi wa kujifunza kwa wengine ili baada ya miaka mitano mpaka kumi uwe umefikia ubobezi wa hali ya juu na kuweza kutangaza uhuru wako na kuondoka chini ya wengine.

SheriaYaLeo; Rejea kwenye hali ya utegemezi ya utoto. Wachukulie wote unaokutana nao wanajua zaidi kuliko wewe na kuwa tayari kujifunza kutoka kwao. Kwa kujiweka kwenye hali hiyo, utajifunza mengi, kwa haraka na kina.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu