2542; Tiba Muda.
Kuna mambo unaweza kuwa unalazimisha yawe kwa namna fulani lakini inashindikana.
Unaweka juhudi za kila aina ili kupata matokeo unayotaka lakini inashindikana.
Unaamua kuachana nayo kwa muda na baadaye unakuja kugundua yamejitatua yenyewe na matokeo yamepatikana bila hata ya kuhangaika sana.
Muda ni tiba ya mambo mengi yanayoonekana kushindikana.
Kwa kuyapa muda wa kutosha, mambo mengi yanajitatua yenyewe.
Ni kuanzia kwenye kazi, biashara na maisha, mambo mengi sana yanahitaji muda kuweza kukaa sawa.
Muda unaponya, muda unaleta ukuaji na muda unaondoa vitu.
Kama kuna majeraha kadiri muda unavyokwenda yanatibika.
Kadiri pia muda unavyokwenda ukuaji zaidi unatokea na hilo kurahisisha mambo.
Na kama yote yatashindikana, basi muda utaondoa au kuua. Maana tunajua kila kitu kina mwanzo na mwisho, kila kitu kitafikia mwisho baada ya muda fulani.
Hatua ya kuchukua;
Kwa jambo lolote linalokusumbua, ambalo umelipa kila aina ya juhudi lakini halijapata majibu, lipe muda. Muda ni tiba nzuri ambayo haijawahi kushindwa, maana hata kama suluhisho halitapatikana, basi muda utalifuta kabisa jambo hilo.
Uweke muda upande wako na hakuna kitakachoweza kukuzuia.
Tafakari;
Ukilazimisha vitu viende vile unavyotaka unazidi kuviharibu na kuvipoteza kabisa.
Ukivipa vitu muda wa kutosha, vitakwenda vizuri kabisa.
Kocha.
Kweli kabisa kocha, vitu vingi vinahitaji muda ili kuweza kwenda vizuri. Kujenga biashara kunahitaji muda, kujenga Mahusiano kunahitaji muda, kutafuta wateja kwenye biashara kunahitaji muda, kuvuka changamoto za maisha kunahitaji muda. Kwa kila kitu tunafanya kwenye maisha yetu kunahitaji muda. Muda ni Tiba kwa mambo mengi kwenye maisha yetu. Ubarikiwe Sana kocha kwa kutukumbusha hili.
LikeLike
Asante Tumaini, kwa hakika bila muda, hakuna maisha wala mafanikio. Tuupe muda thamani ya kutosha.
LikeLike