#SheriaYaLeo (46/366); Umakini kwenye kujifunza haujawahi kushindwa.
Japo inaweza kuonekana inachukua muda mrefu kwenye kujifunza mpaka kufikia ubobezi wa hali ya juu, umakini, juhudi na muda unaowekwa kwenye kujifunza haupotei.
Tafiti zilizofanywa kwenye eneo la ubobezi zinaonyesha kwamba mtu anahitaji kujifunza na kufanya kwa umakini mkubwa kwa angalau masaa elfu kumi ndiyo afikie ubobezi wa hali ya juu.
Hicho ni kipindi cha miaka 7 mpaka 10 ya kujifunza kupitia ufanyaji kwa umakini mkubwa.
Huo ndiyo muda unaohitajika kwenye kila eneo ambalo mtu anataka kujijengea ubobezi.
Kwa kuwa ni muda mrefu, wengi huchoka na kuona wanapoteza muda, hivyo kuacha kile walichokuwa wanafanya na kuhangaika na mambo mengine.
Wewe usiwe hivyo, weka umakini mkubwa kwenye kujifunza kwa kufanya ukijua muda na juhudi unazoweka hazipotei.
Bali vyote vinajikusanya na kuja kuzalisha matokeo makubwa pamoja na ubobezi wa hali ya juu.
Ondoka kwenye kundi kubwa la watu ambalo linataka matokeo ya haraka kwenye kile wanachofanya la sivyo wanakata tamaa.
Wewe jipe muda wa kutosha na weka umakini wako mkubwa ukijua hakuna kinachoweza kupotea.
Sheria ya leo; Weka muda wa kutosha kwenye kujifunza na kufanya kwa umakini mkubwa. Rudia hilo bila kuchoka mpaka utakapofikia ubobezi wa hali ya juu.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu