2544; Hujuma.

Kama unaweka juhudi kubwa ili uweze kufanikiwa, lakini juhudi hizo hazileti matunda mazuri na kila wakati unakutana na vikwazo na magumu mbalimbali, jua kuna hujuma zinaendelea.

Kuna nguvu kubwa inayopinga kila juhudi unazoweka na ndiyo maana hupati matokeo mazuri.

Hujuma zinaweza kuwa zinatoka ndani yako mwenyewe au kutoka kwa wengine.
Na pia zinaweza kuwa zinafanywa kwa makusudi au bila ya mtu kujua.

Chochote kinachopinga juhudi kubwa unazoweka ili ufanikiwe ni hujuma, kama hutazikabili waziwazi hujuma hizo, hutaweza kufanikiwa.

Kuna kipindi kampuni ya magari ya umeme ya Tesla ilikuwa inachelewesha uzalishaji kulingana na ahadi zake. Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Elon Musk aliamua kuwa anashinda na kulala kwenye kiwanda, huku kila siku akitangaza lazima afukuze baadhi ya watu kazi. Alieleza kabisa kwamba kwa juhudi kubwa wanazoweka, kama matokeo hayapatikani kuna watu wanahujumu. Na jukumu lake kubwa ni kuwajua wahujumu hao na kuwaondoa. Hilo lilimwezesha kuongeza uzalishaji na kufikia lengo.

Hatua ya kuchukua;
Kwa kila jambo lako linalokwama, usiridhike tu kwa kujiambia mambo ni magumu. Bali jiulize ni hujuma gani zinaendelea kwenye hiyo. Utakapodadisi kwa kina, utajionea mwenyewe nguvu ambazo zinakinzana na juhudi unazoweka.
Ukishagundua nguvu hizo, usizilazie damu, hakikisha unaziondoa haraka ili juhudi unazoweka ziwe na tija.

Tafakari;
Hakuna nguvu na juhudi zinazoweza kupotea kama hakuna ukinzani unaozipoteza. Hujuma ndiyo njia kubwa inayotumika kuzuia nguvu na juhudi kubwa ambazo mtu anaweka kwenye kile anachofanya. Jua jinsi ya kutambua na kuondokana na hujuma ili zisiwe kikwazo kwako.

Kocha.