2545; Kuwa fursa inayotafutwa.

Kwenye maisha kuna watu wa aina mbili.

Aina ya kwanza ni wale ambao kila wakati wanatafuta fursa mpya.
Kila wakati kuna kitu kipya wanafanyia kazi.
Hawakai kwenye kitu kimoja kwa muda mrefu, kwa sababu wanaposikia kuna kingine kipya na kizuri zaidi, wanaacha walichokuwa wanafanya na kwenda kwenye hicho kingine.
Watu hawa huwa hawapigi hatua kubwa, wanahangaika na mengi lakini watabaki pale walipo miaka yote.

Aina ya pili ni watu ambao wanatafutwa kama fursa. Hawa ni watu ambao wamefikia ubobezi mkubwa kwenye kile wanachofanya na wanaotoa thamani kubwa mno kiasi kwamba kila mtu anataka kufanya nao kazi.
Watu hawa huwa wanafikia ubobezi huo baada ya kuwa wamekaa kwenye kitu kimoja kwa muda mrefu, wakikifanya kwa umakini mkubwa na kujifunza kwa kina.
Wanakuwa wanakijua kitu hicho nje ndani, wakiweza kukifanya kwa viwango vya juu kabisa.

Kama unavyoona hapo, kinachotofautisha aina hizo za watu ni kitu kimoja tu, kuchagua kitu kimoja na kujitoa kweli ili kukibobea badala ya kuhangaika na vitu vipya kila wakati.
Ni kitu ambacho kinaweza kufanywa na kila mtu, lakini ni wachache sana watakaokifanya.
Kuwa mmoja wa hao wachache.

Hatua ya kuchukua;
Kama hujachagua kitu kimoja ambacho unakwenda kubobea, kichague sasa.
Kama umeshachagua, fumba macho yako kwenye fursa nyingine mpya zinazojitokeza kila wakati.
Pamoja na usawishi wake mkubwa, hazina manufaa kuliko ubobezi utakaojenga.
Jijengee ubobezi na utakuwa fursa inayotafutwa na wengine, badala ya wewe kuwa mtafuta fursa kila wakati.

Tafakari;
Tunapenda kukimbizana na vitu vipya kila wakati. Lakini watu tunaowakubali na ambao ni mashujaa wetu, huwa wanakaa kwenye kitu kimoja kwa muda mrefu mpaka wanabobea. Chagua unataka upande upi.

Kocha.