#SheriaYaLeo (49/366); Aina mbili za kushindwa.

Kuna aina mbili za kushindwa.

Aina ya kwanza ni kushindwa kabla hata ya kuanza.
Hapa unahofia kufanya kwa sababu unaona utashindwa au kwa sababu unaona bado muda haujawa sahihi, hujawa na maandalizi ya kutosha.
Kwenye aina hii ya kushindwa hakuna chochote unachojifunza.
Woga wako wa kujaribu unakuharibu kabisa.

Aina ya pili ni kushindwa baada ya kuchukua hatua kubwa na za kijasiri.
Kwenye aina hii ya kushindwa unajifunza mengi kwa hatua ambazo umechukua.
Unajua ni kitu gani unapaswa na hupaswi kufanya wakati mwingine.

Kadiri unavyoendelea kushindwa kwa kufanya, unajifunza na kuwa imara zaidi. Unazidi kuwa imara kwenye kujaribu mambo makubwa na kujifunza zaidi.

Kushindwa kwa kufanya ni zawadi nzuri kwenye kile unachofanya, maana inakupa nafasi ya kujifunza na kuwa bora zaidi.
Kutokushindwa kwa mara ya kwanza ni kama laana kwako, maana hutajifunza, utavimba kichwa kwa kujiona unajua sana na hilo litapelekea upate anguko kubwa sana baadaye.

Kutokushindwa kwa mara ya kwanza kutakuzuia usione bahati ambayo imehusika hivyo pale unapokuja kushindwa baadaye utashindwa kuelewa au kujifunza chochote.

Kwa chochote unachofanya, jaribu mawazo mapya na makubwa mapema, utashindwa katika hayo, lakini utapata funzo kubwa ambalo litakusaidia kufanya makubwa zaidi.

Sheria ya leo; Ni bora ufanye na ushindwe kuliko kutokufanya kabisa. Leo nenda kuchukue hatua kwenye moja ya mawazo makubwa uliyonayo. Utashindwa, lakini utajifunza mengi yenye manufaa kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu