2547; Safari ya mafanikio haitofautiani na maisha.

Kwenye maisha, huwa tunajua jinsi vitu vilivyo na kuenda navyo kwa namna vinavyoenda.

Kama umeoa au kuolewa, umekaa na mwenza wako kwa muda mrefu na mtaendelea kukaa kwa muda mrefu.
Hukai naye ukijiambia kuna kitu fulani unataka kukipata kisha kutokuendelea naye tena. Mwenzako no sehemu ya maisha yako.

Kama una mtoto/watoto, umewalea kwa muda mrefu na utaendelea kuwalea kwa muda mrefu zaidi. Hufikirii kwamba utawalea watoto wako kama watakubali na kama watakataa basi unaachana nao.
Huwalazimishi watoto wakue haraka ili umalizane na wajibu wa kulea, bali unaenda nao kama wanavyokwenda.

Hiyo ni mifano michache, lakini inakupa picha jinsi maisha yanavyoenda, tunachagua vitu na kuvipokea kuwa sehemu ya maisha yetu, kwa kipindi chote cha maisha.

Sasa inaposhangaza ni inapokuja kwenye safari ya mafanikio.
Huwa tunategemea mambo yaende haraka kwa kadiri ya matakwa yetu.
Huwa hatuna kujitoa kwenye kitu kwa maisha yetu yote, tupo tayari kukiacha kitu haraka pale ambapo hakileti matokeo ambayo tunayataka.

Mwishowe ni tunajikuta tumehangaika na mambo mengi na hakuna matokeo yoyote makubwa tumeyapata, hakuna mafanikio tuliyojenga.

Hatua ya kuchukua;
Unapoingia kwenye safari ya mafanikio, jua ni safari ya maisha. Wajibu wako ni kukaa kwenye mchakato sahihi, kujifunza yaliyo sahihi, kuchukua hatua sahihi na kuendelea kuboresha kadiri unavyokwenda.
Matokeo yatakuja yenyewe na kwa wakati wake. Wewe wajibu wako ni kukaa kwenye mchakato.

Tafakari;
Safari ya mafanikio ni sawa na safari ya maisha, huwezi kuilazimisha iende unavyotaka wewe. Hakuna njia za mkato. Na siyo kitu cha kufikia na kuwa umemaliza. Ni zoezi endelevu, lenye hatua kubwa za kuendelea kupiga kila wakati.

Kocha.