#SheriaYaLeo (51/366); Elewa jinsi ubongo unavyofanya kazi.

Huwa tunadhani tunaweza kuruka hatua, kuepuka mchakato, kutumia kanuni rahisi au vipaji vyetu kufikia ubobezi kwa muda mfupi bila kuweka kazi.

Ujio wa teknolojia umetufanya tuone kuna namna tunaweza kuukwepa mchakato mzima wa ubobezi.
Kwa sababu teknolojia zimerahisisha mengi, tunadhani zinaweza pia kurahisisha mchakato wa kujifunza na ubobezi.

Lakini sivyo uhalisia ulivyo.
Ubongo wetu binadamu bado unafanya kazi kwa namna ile ile na hakuna njia ya mkato unayoweza kutumia.
Bado ubongo wetu unahitaji muda, umakini mkubwa na kurudia rudia kwa muda mrefu ndiyo uweze kujifunza kitu na kufikia ubobezi.

Kadiri tunavyohangaika na njia za mkato na kuuacha mchakato sahihi, ndivyo tunavyozidi kuwa dhaifu kadiri muda unavyokwenda.
Tunanasa kwenye kazi au biashara ambazo hazina fursa ya ukuaji.
Tunakuwa watumwa wa maoni na hofu za wengine.

Badala ya akili kutuunganisha na uhalisia, tunatengana nao na kujifungia kwenye chumba cha fikra zetu finyu.
Tunakuwa tumefunga uwezo mkubwa wa akili zetu kujifunza na kufanya makubwa na kuishia kuhangaika na kila aina ya usumbufu, tukishindwa kufikiri kwa kina na kuwa na umakini.

Pamoja na mabadiliko makubwa ya teknolojia yanayoendelea, ubongo wetu binadamu bado unafanya kazi kwa namna ile ile.
Tunapaswa kutumia namna hiyo na kuacha kuhangaika na njia za mkato zisizokuwa na manufaa yoyote.
Ni lazima uweke muda, juhudi na umakini katika kujifunza na kufanya ndiyo uweze kufikia ubobezi wa juu.

Sheria ya leo; Weka imani yako kwenye kujifunza na siyo kwenye teknolojia. Kama hutaweza kujifunza kwa kina na kufikia ubobezi, teknolojia zitaishia kukupoteza badala ya kukusaidia.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu