2548; Kutulia siyo tu kwenye kile unachofanya, bali na kwenye maisha pia.
Tumezungumza mara nyingi hapa umuhimu wa kuchagua fursa moja na kutulia nayo kwa muda mrefu ndiyo uweze kupata matunda mazuri.
Tunapaswa kuacha kuhangaika na kila fursa mpya, maana huko ni kupoteza nguvu kusiko na tija.
Wapo wanaofanya hivyo, lakini bado wanashindwa kubobea na kufanya makubwa kwenye kile walichochagua.
Na hiyo ni kwa sababu wanatawanya nguvu zao nyingi kwenye mambo mengine ya maisha yao kiasi kwamba hawapati muda wa kutosha kuweka kwenye kile wanachofanya.
Lengo la kuchagua kimoja kati ya vingi ni usitawanye nguvu zako, uweke juhudi zako zote kwenye kile unachofanya ili uweze kufanya makubwa.
Sasa kama utaokoa nguvu kwa kupunguza yale unayoyafanya, halafu ukaishia kuzipoteza kwenye mambo mengine ya kimaisha, inakuwa haina maana.
Nguvu unazopoteza zinakuwa kikwazo kwako kufanikiwa.
Kama unajihusisha na starehe nyingi, ni mlevi, una mahusiano mengi na unahangaika sana na maisha ya wengine, yote hayo yanakugharimu muda na nguvu, ambazo huwezi kuzitumia kwa mafanikio.
Kama unatumia muda mwingi kuperuzi mitandao, kufuatilia habari na kubishana mambo mbalimbali unajiweka kwenye hasara.
Na hata kama una maamuzi mengi ya kufanya kwenye siku yako, kuanzia utafanya nini, utavaa nini, utakula nini na kadhalika, yote hayo yanaigharimu akili yako na kutumia vibaya rasilimali zako muhimu.
Kuna sababu kwa nini dini na falsafa mbalimbali huwataka watawa wake kuwa na maisha rahisi na yasiyo na mambo mengi.
Kuna sababu kwa nini mabilionea wengi huvaa mavazi ya kawaida na ya aina moja, hula chakula cha aina moja hawana mahusiano mengi, ya kimapenzi na hata ya kirafiki.
Kuna sababu kwa nini kila hadithi ya aliyefikia ubobezi wa hali ya juu sana inaeleza jinsi ambavyo alipuuza mengine yote na kuweka umakini wake wote kwenye kitu kimoja tu.
Wapo ambao hawakuwa hata wanakula kwa muda, wengine hawakuwa wanapata muda wa kuoga mara kwa mara.
Kile walichokuwa wanafanya kiliwameza moja kwa moja na hilo ndiyo liliwawezesha kufikia ubobezi wa hali ya juu.
Hatua ya kuchukua;
Yarahisishe sana maisha yako, punguz sana maamuzi unayopaswa kufanya kwenye siku yako. Zifanye siku zako zifanane na kuwa rahisi.
Ukiamka unajua kabisa kipi kikuu unachokwenda kufanya.
Punguza kufikiria kuhusu utavaa nini, utakula nini na utakutana wengine saa ngapi. Kuwa na vitu rahisi vinavyijirudia kila siku ili upunguze maamuzi na kuweka nguvu zako zote kwenye kile unachofanya.
Tafakari;
Kila maamuzi unayofanya kwenye siku yako, yanatumia sehemu ya nguvu zako na hivyo kukuchosha zaidi. Kama siyo maamuzi yanayohusiana na kile muhimu unachofanya, ni matumizi mabaya ya nguvu zako, ambayo hayakuletei tija yoyote.
Kocha.