#SheriaYaLeo (52/366); Tengeneza Kuhitajika.

Wakati unajijengea ubobezi wako, tengeneza kuhitajika kwako na watu wengine.

Wafanye wale unaowalenga kwenye kile unachofanya wakutegemee wewe zaidi.
Hakikisha bila uwepo wako kuna mambo muhimu wanakosa au vitu vyao muhimu vinakwama.

Hili ni muhimu sana kwa sababu kadiri unavyobobea ndivyo unavyozidi kutoza gharama kubwa kwenye kile unachofanya.
Wakati huo kuna wengine wengi ambao watakuwa wanafanya unachofanya, ila kwa kuwa hawajafikia ubobezi kama wako, wanatoza gharama ndogo.

Sasa kama hakuna kitu watu wanategemea kwako, kama wanaweza kupata kwa wengine kile wanachopata kwako, hawatajali umekuwa nao kwa muda gani na umewasaidia kwa kiasi gani, watakuacha na kwenda kwa wengine ambapo ni rahisi zaidi.

Hivyo salama yako kubwa wakati unajijengea ubobezi, njia pekee ya kuendelea kupata kazi na kipato kikubwa ni kuwafanya wengine wakutegemee wewe kwa kiasi kikubwa.
Wape thamani kubwa sana ambayo hawawezi kuipata sehemu nyingine yoyote na hiyo itawafanya waendelee kufanya kazi na wewe bila ya kujali gharama unazotoza.

Kumbuka sisi binadamu ni wabinafsi na tunaangalia namna gani tunanufaika sisi wenyewe kwanza kabla hatujaangalia wengine.
Kama hakuna ambacho watu wananufaika nacho kupitia wewe, ambacho hawawezi kukipata kwa wengine, hakuna kitakachowasukuma kuja kwako.

Sheria Ya Leo; Kazana kuwa mtu pekee unayeweza kufanya ulichochagua kwa upekee na kuwafanya wale unaowalenga wakutegemee wewe kwa kiasi kikubwa katika kukamilisha mambo yao.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu