2554; Akili ‘itajiseti’ yenyewe.

Akili zetu sisi binadamu zina uwezo mkubwa mno, uwezo ambao hatuwezi hata kuuelewa.

Mara nyingi huwa tunafikiria baadhi ya mambo yakitokea basi maisha yetu yatavurugika sana.

Labda ni kifo cha mtu wa karibu tunayemtegemea sana.
Labda kufukuzwa kazi au biashara zetu kufa.
Labda kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine.
Labda kupata maradhi sugu au ulemavu ambao unatubadili kabisa.

Kabla ya mambo kama hayo kututokea, huwa tunaona yakitokea basi maisha hayataweza kwenda tena, au yatakuwa magumu kupitiliza.

Na kweli pale mambo hayo yanapotokea, maisha yetu yanabadilika sana na kinakuwa kipindi kigumu kuyakabili mambo hayo.
Tunakuwa kwenye hali ya mshtuko mkubwa na kutokujua tufanyeje.

Lakini kadiri muda unavyokwenda, tunazoea hali hizo mpya na akili zetu zinajiseti upya.
Haichukui muda sana tunakuwa tumerudi kwenye hali yetu ya kiakili kama ilivyokuwa kabla ya jambo kutokea.

Na hata kiwango cha furaha, kinarudi mahali pake baada ya muda fulani kupita, bila kujali umekutana na tukio gani.

Tafiti zinaonyesha hata watu waliopata ulemavu wa kudumu, baada ya muda fulani hali yao ya furaha inarudi kwenye kiwango cha awali. Akili yao inakuwa imejiseti na kurudi kwenye ukawaida wao, bila ya kujali nini kimetokea.

Kwa kujua hili, tunapata uhuru mkubwa.
Tunaweza kuacha kuhofia kama mambo fulani yakitokea maisha yataendaje.
Kwa kujua kama bado tutakuwa hai, akili zetu zitajiseti na maisha yataendelea.

Hatua ya kuchukua;
Kila unapofikiria na kuhofia kwamba jambo fulani likitokea basi litavuruga sana maisha yako, jiambie hata likitokea, akili itajiseti na maisha yataendelea.
Hivyo kuwa huru kuishi kwenye wakati uliopo na kufurahia kitu au watu wakati bado upo navyo.

Tafakari;
Kama bado upo hai, hakuna jambo lolote linaloweza kutokea kwenye maisha yako na kuyavuruga kabisa. Mwanzo jambo litakutikisa, lakini baada ya muda akili itajiseti na maisha yataendelea.

Kocha.