2568; Uhakika upo kwenye mchakato.
Ukienda kununua baadhi ya vifaa, mfano simu, tv, redio n.k, huwa unapewa uhakika.
Kwamba kifaa hicho kitafanya kazi vizuri na kama kitakuwa na shida basi unaweza kukirudisha na kupewa kingine.
Hii ni njia ya masoko ambayo imekuwa na nguvu kwa sababu binadamu tunapenda sana uhakika.
Na hilo tumelihamishia kwenye maeneo mengine ya maisha yetu, tunataka kuwa na uhakika kwenye kila kitu.
Mbaya zaidi ni tunataka uhakika kwenye vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wetu. Mfano kutaka uhakika wa matokeo kwenye chochote unachofanya.
Asili haijawahi kuwa na uhakika wa matokeo. Unaweza kuwa na mipango mizuri sana ya kesho, lakini huwezi kuwa na uhakika na kesho. Unaweza usiwepo hiyo kesho au mambo mengine yanaweza kutokea na kuvuruga mipango yako.
Kuna matokeo yanaweza kuwa yanatokea yenyewe halafu tukadhani yametokea kwa sababu ya uhakika wetu. Tunaweza kudanganyika na matokek ya aina hiyo mpaka pale tunapokutana na uhalisia na kuumia sana. Pale tunapotegemea kwa uhakika matokeo fulani halafu yakaja mengine, ule uhakika tunaokuwa tumejipa unatuumiza sana.
Kitu pekee unachoweza kuwa na uhakika nacho kwenye safari yako ya mafanikio ni mchakato unaofuata. Zile hatua unazochukua na juhudi unazoweka ndiyo kitu ambacho una uhakika nacho.
Matokeo ni kitu ambacho huna uhakika nacho. Unaweza kutegemea matokeo ya aina fulani, lakini uhakika wa lini utayapata na kwa kiwango gani huwezi kuwa nao.
Weka nguvu na umakini wako kwenye vitu vilivyo ndani ya uwezo wako na kikubwa ni mchakato wako.
Pambana na mchakato na yaache matokeo yaje kwa wakati wake.
Unapotaka kuwa na uhakika wa matokeo au kulazimisha matokeo ya aina fulani ndipo unapoingia kwenye njia zisizo sahihi ambazo zitakugharimu zaidi.
Hatua ya kuchukua;
Ni uhakika gani ambao umekuwa unautaka sana kiasi cha kutoka kwenye njia sahihi kwa mafanikio yako? Pale unapoingia kwenye njia za mkato na kuhangaika na yasiyo sahihi ni matokeo ya kutafuta uhakika ambao haupo.
Wewe jua uhakika wako upo kwenye mchakato na huo ndiyo unaopaswa kuupa kipaumbele na kuweka juhudi zako zote.
Tafakari;
Kila jambo lina mchakato na matokeo. Mchakato upo ndani ya uwezo wako, matokeo yako nje ya uwezo wako. Pambana na mchakato, matokeo yatakuja yenyewe.
Kocha.