#SheriaYaLeo (73/366); Jijengee ustahimilivu.

Safari ya kuelekea kwenye ubobezi wa hali ya juu na mafanikio makubwa siyo rahisi.
Kadiri unavyokwenda ndivyo inataka zaidi kutoka kwako, ikitaka muda wako na juhudi zako zaidi na zaidi.

Hilo huwachosha wengi na kuamua kuishia njiani, maana hujikuta wanaishiwa nguvu na kuchoka sana.

Kama wewe unataka kuendelea na safari hii bila kuchoka, lazima ujijengee ustahimilivu mkubwa.
Lazima uendelee kuweka muda, nguvu na juhudi kubwa kwa muda mrefu bila kuacha.

Na hapo ndipo afya yako ya mwili inapokuwa muhimu sana kwenye hii safari.
Bila afya bora ya mwili, hutaweza kudumu kwa muda mrefu kwenye hii safari.
Kama kila mara una maradhi au uchovu uliopitiliza, hutaweza kutoa kama safari inavyotaka ikutoe.

Hivyo ili kujenga ustahimilivu, unapaswa kujenga na kulinda sana afya yako ya mwili.
Na hilo linafanyika kwa kuzingatia mambo matatu muhimu.

Moja ni ulaji wako, usiweke vyakula na vinywaji visivyo sahihi kwenye mwili wako. Sukari, wanga kwa wingi na vilevi vya aina yoyote ile ni vitu vya kuepuka kabisa.

Mbili ni mazoezi, unapaswa kuwa na mpango wa mazoezi ya mwili wa kila siku. Kadiri unavyofanya mazoezi zaidi ndivyo mwili wako unavyotengeneza nguvu zaidi na hilo kukupa ustahimilivu mkubwa.

Tatu ni kupumzika, mwili wako siyo mashine, unahitaji mapumziko ili kukusanya nguvu zake na kuweza kuendelea na safari. Hivyo hakikisha umapata muda wa kutosha wa kupumzika.

Ni muhimu sana uuchukulie mwili wako kimkakati, ili mara zote uwe kwenye afya njema ya kuweza kuendelea na safari ya ubobezi na mafanikio licha ya ugumu na changamoto zake.

Sheria ya leo; Kutengeneza kitu chochote chenye thamani kunahitaji muda, nguvu na juhudi kubwa. Ni lazima uwe na maandalizi sahihi ya kukuwezesha kustahimili ugumu na urefu wa safari.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji