2573; Hakuna kisicho na manufaa.
Kwenye maisha yetu, huwa tunapitia mambo mbalimbali kwa nyakati mbalimbali.
Baadhi ya mambo hayo yapo ndani ya uwezo wetu, huku mengi yakiwa nje ya uwezo wetu.
Kwa tafsiri zetu wenyewe, kuna baadhi ya mambo tunasema ni mazuri huku mambo mengine tukisema ni mabaya.
Kama yanaendana na tunachotaka tunaona ni mazuri kwetu.
Na kama hayaendani na tunachotaka tunaona ni mabaya.
Ambacho tunasahau ni kwamba mambo huwa yanatokea kama yanavyotokea, siyo mazuri wala mabaya.
Tafsiri ya uzuri au ubaya wa jambo inatokana na mtazamo wetu wenyewe.
Muhimu zaidi tunachopaswa kuzingatia kwenye kila jambo ni kwamba halikosi matumizi.
Kila kinachotutokea, bila kujali tumekitafsiri kama kizuri au kibaya huwa kina manufaa fulani ndani yake.
Lakini manufaa hayo huwa hayapo wazi, huwezi kuyaona mpaka pale utakapoyatafuta kwa makusudi na kuweza kuyatumia.
Hata jambo unaloona ni baya kabisa, labda limekuumiza sana, tambua kuumia huko kuna manufaa kwako. Kwani kunakufanya kuwa imara zaidi na usiweze kuumizwa na vitu vingine vya aina hiyo.
Hatua za kuchukua;
Kwa kila kitu kinachotokea au unachokutana nacho, jiulize ni manufaa gani yako ndani yake. Weka pembeni tafsiri yako ya uzuri au ubaya na tafuta manufaa yaliyo ndani ya kitu hicho. Utayaona manufaa hayo na ukiweza kuyatumia vizuri, utaweza kupiga hatua zaidi.
Tafakari;
Kila kitu kinachotokea kwenye maisha yako ni rasilimali ya kujenga maisha bora zaidi. Usipoteze chochote kupitia tafsiri zako binafsi kwenye vitu hivyo, wewe angalia manufaa yako wapi na yatumie hayo.
Kocha.