#SheriaYaLeo (77/366); Ubobezi Na Mafanikio Haviji Kirahisi.
Kutengeneza kazi yoyote ya kibunifu na yenye maana au kufanya ugunduzi wa kitu kipya inahitaji nidhamu ya hali ya juu, kuweza kujidhibiti na utulivu na uimara wa kihisia.
Inahitaji sana mtu kuweza kubobea kwenye kila eneo linalohusika na kile anachofanya.
Nguvu hizo haziwezi kuja kirahisi na kupitia njia za mkato kama wengi wanavyojidanganya na madawa na vitu vingine.
Unapowaangalia wale waliofikia ubobezi na mafanikio makubwa, tambua kwamba wameweka juhudi kubwa kwa muda mrefu bila kuchoka. Wamekuwa na utararibu wa kujifunza na kufanya kwa kurudia rudia bila kuacha. Na wamekutana na vikwazo na magumu mbalimbali ambayo hawakukubali yawarudishe nyuma, badala yake walikabiliana nayo mpaka kuyavuka.
Kama na wewe unataka kufikia ubobezi wa hali ya juu na mafanikio makubwa, lazima ujue wazi kabisa kwamba safari hiyo haitakuwa rahisi. Lazima ujiandae kwa kila namna na kuwa tayari kuendelea na mapambano bila kuacha mpaka ufike na kupata unachotaka.
Sheria ya leo; Nguvu ya ubunifu ni matunda ya juhudi kubwa ambazo mtu ameweka kwa muda mrefu. Usijidanganye kwamba kuna njia rahisi na ya mkato ya kufikia nguvu hiyo.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji