2574; Mgongo ukutani.
Kama unapigana na mtu, ambaye unaona ni vigumu kumshinda, unaweza kuwa unarudi nyuma kama sehemu ya kumkwepa.
Kama utarudi nyuma mpaka kujikuta mgongo umekutana na ukuta, hapo unajua wazi hakuna tena njia ya kukimbia.
Ni labda upambane kwa kila namna ushinde au ushindwe vibaya.
Unapokuwa katika hali ya aina hiyo, kuna nguvu kubwa sana ambayo huwa inakujia na kukusukuma kupambana kwa kila namna.
Mara zote unapokuwa na machaguo mengi, unatawanya nguvu zako sana na hivyo kushindwa kupambana kweli kweli kwenye kitu kimoja.
Machaguo hayo yanapoondoka, nguvu zako zote zinabaki kwenye chaguo moja na hivyo kuweza kulifanyia kazi vizuri na kwa kina mpaka lilete matokeo mazuri.
Kama kuna mafanikio unayataka na hujayapata kwa muda mrefu, hebu jiangalie kama kweli umeweka mgongo wako ukutani.
Angalia kama kweli umeachana na machaguo mengine na kuweka nguvu zako zote kwenye kitu hicho.
Hapo ndipo wengi hukwama, kwa kuhangaika na mambo mengi, wanashindwa kufanikiwa kwenye jambo lolote moja.
Hatua ya kuchukua;
Weka mgongo wako ukutani, ondoa kila njia ya kutoroka kile unachotaka kufanikiwa na kifanye kuwa kipaumbele cha kwanza kwako.
Tafakari;
Muda, nguvu na umakini ni rasilimali zenye ukomo. Kadiri unavyozitawanya kwenye mambo mengi ndivyo unavyojizuia kufanikiwa. Chagua eneo moja au machache sana ambapo utawekeza rasilimali hizo vizuri mpaka upate tija.
Kocha.