2580; Ngoma Droo.
Kwenye wimbo wake wa Bongo Dar es Salaam, msanii Profesa Jay aliimba mashairi haya;
“Aliyeuziwa cheni katoa hela bandia,
Aliyepokea hela nae kauza cheni ya bandia.
Tuliozoea jiji tunasema ngoma droo.”
Kuna ngoma droo nimekuwa naiona kwenye upande wa safari ya mafanikio, ambayo kama mtu hutaweza kuivunja basi hutaweza kufanikiwa.
Kitu kikubwa ambacho nimekuwa nakiona ni hiki;
Wale wanaouza bidhaa au huduma mbalimbali, wanalalamika kwamba wanunuaji hawapo tayari kulipa bei kubwa. Hivyo wanauza kwa bei ndogo na hivyo hawapati faida nzuri.
Huku wale wanaonunua bidhaa na huduma hizo wakilalamika kwamba hawapati thamani nzuri. Haziwapi kile ambacho walikuwa wanataka, hivyo kujikuta wakinunua kwa wingi lakini bado hawanufaiki.
Na hapo ndipo penye ngoma droo, muuzaji hapati faida na mnunuaji hapati thamani.
Ili kutoka kwenye mkwamo huo, lazima mmoja avunje hali hiyo. Na ni rahisi kwa muuzaji kuanza kuivunja, kwa kutoa thamani kubwa kwa bei ambayo itampa faida nzuri.
Kisha kutafuta wateja sahihi wanaoielewa thamani hiyo. Wateja hao wanapopata thamani kubwa, wanakuja tena na tena na hata kuleta wengine.
Hatua ya kuchukua;
Kwa chochote unachouza, iwe ni huduma, bidhaa, ujuzi n.k, kazana kutoa thamani kubwa sana na toza gharama zitakazokuwezesha upate faida nzuri. Usihofie kukosa wateja, wapo, ila utahitaji kuweka juhudi kubwa mwanzoni ili kuwapata. Baada ya kuvuka ugumu wa mwanzoni, mambo yatakwenda vizuri.
Tafakari;
Unaweza kutoa thamani kubwa kwa wachache na wakakulipa vizuri au ukatoa thamani ndogo kwa wengi na wakakulipa kidogo. Uchaguzi ni wako.
Kocha.