2583; Wateja.
Kuna wateja wanajua thamani ya kile unachouza au kufanya, ambao wapo tayari kulipia mara moja na kupata thamani hiyo.
Wateja hawa siyo wasumbufu na wananufaika kweli na kile unachowauzia.
Kuna wateja ambao wanaona unatoza sana na hivyo kutaka uwapunguzie. Watalalamika sana, wakionekana wanakihitaji kweli kitu ila kinachowakwamisha ni bei.
Unaweza kushawishika kuwapunguzia bei, lakini hilo bado halitawaridhisha, kwani hata wakinunua bado wataendelea kukusumbua wakitaka wapate zaidi na zaidi.
Halafu kuna wateja ambao hawajali, hata ufanye nini, bado watakuwa hawajali.
Wanaweza kukupa sababu mbalimbali, labda bei, labda wanataka aina nyingine.
Lakini hata ukiwapunguzia bei au kuwaletea hiyo aina nyingine, bado hawatanunua, wataendelea kuja na sababu lukuki.
Kwa kuwa watu wengi wanapenda kufanya biashara kiurahisi, huwa wanakimbilia kuhangaika na wateja wengi ambao hawaioni thamani au hawajali. Hilo linayafanya maisha yao ya kibishara kuwa magumu kwani kila wakati kuna mahangaiko na wateja.
Hatua ya kuchukua;
Watenge wateja wako kwenye makundi hayo matatu, kisha endelea kuwahudumia wote.
Halafu mpango wako unakuwa huu, kazana kuongeza wateja wapya wawili wanaoielewa thamani na ukishakamilisha hilo, punguza mmoja asiyeelewa thamani.
Nenda hivyo kwa muda na utashangaa jinsi hali yako ya biashara itakavyobadilika.
Hilo litahitaji kazi kubwa sana, lazima uwe tayari kuiweka.
Tafakari;
Haiwezekani watu wote wakaelewa kile unachofanya. Hivyo achana na mpango wa kutaka kueleweka na kila mtu na chagua wale wanaokielewa vyema unachofanya kisha ujenge nao mahusiano mazuri.
Kocha.