#SheriaYaLeo (88/366); Nenda zaidi ya akili.

Wakati wa kuanza kufanya kitu, mtu anatumia zaidi akili kufikiri na kufanya.
Hilo linapelekea mtu kufanya kwa namna ambayo wengine pia wanafanya.

Ni baada ya kufikia ubobezi wa hali ya juu ndiyo mtu anakuwa amezama kweli kwenye kile anachofanya, kiasi kwamba ufanyaji unakuwa sehemu yake.
Hatumii tena akili kufikiri kufanya, ufanyaji unakuwa sehemu ya maisha yake.

Kwa njia hii anajikuta akiweza kufanya kitu kwa kina zaidi, tofauti na wengine wanavyofanya.
Pia anakuwa na uelewa mkubwa wa kitu, kwa sababu anakuwa kama ndiyo kitu hicho.

Hii ni hatua muhimu unayopaswa kupiga ili uweze kufika kwenye ubobezi wa hali ya juu, kuzama kweli kwenye kile unachofanya kiasi cha kitu hicho kuwa sehemu yako na kuweza kukifanya bila ya kutumia akili.

Hii haimaanishi unafanya kwa mazoea, bali machale yako yanakuwa sahihi kwenye kitu hicho.
Pale ambapo kipo sawa au hakipo sawa unajua kabisa, hata kama huwezi kuelezea ni kwa sababu gani.
Wakati wengine wanakiona kitu kwa juu juu, wewe unakiona kwa kina kabisa.

Sheria ya leo; Baada ya muda wabobezi huwa wanazama kwa kina kwenye kile wanachofanya kiasi cha kuwa sehemu yao na kutohitaji kutumia akili na kufikiri sana kwenye kukifanya. Hilo unaweza kulifikia pia kama utazama kwa kina kwenye kile unachofanya na kuwa na subira, ung’ang’anizi na uvumilivu.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji