2586; Ufalme wa mteja.
Kauli maarufu sana kwenye biashara ni mteja ni mfalme.
Wengi husema tu kauli hiyo bila kufikiri kwa kina na kuelewa maana yake.
Kuielewa kauli hiyo ni vyema kuanza na sifa za mfalme.
Mfalme ni mtu wa aina gani?
Ni mtu mwenye kauli ya mwisho na anayepata kile anachotaka bila kubishiwa.
Na hizo ndiyo sifa kuu za mteja wa biashara yako.
Mteja ndiye mwenye kauli ya mwisho, maana ndiye mwenye fedha, asipoamua kununua kwako huwezi kumlazimisha.
Lakini pia mteja ana nguvu ya kupata anachotaka, kwa sababu ana fedha. Akikosa kwako atakwenda kwa mwingine.
Unapoelewa hili kwa kina unagundua kazi kubwa kwenye biashara yako ni kumtumikia mteja wako ambaye ni mfalme.
Kumsikiliza kwa makini ili kujua nini anataka na kisha kumpatia kile anachotaka.
Usimlazimishe kile unachotaka wewe, bali mpe kile anachotaka yeye.
Muhimu sana kwenye biashara ni kuwapa wateja kile ambacho tayari wanakihitaji.
Ndiyo, kitakuwa ni kitu ambacho wengine wanawapa pia,
Ila wewe unapaswa kuwapa kwa namna ambayo hawajawahi kukipata kutoka kwa wengine.
Na hapo ndipo mteja anapojiona mfalme kweli, anapoacha kwenda kwa wengine na kuja kwako, kwa sababu anajua kwako atapata ambacho hawezi kupata kwa wengine.
Hatua ya kuchukua;
Ni kwa namna gani biashara yako inamfanya mteja kujisikia ni mfalme kweli?
Fanyia kazi hili ili wateja wapate msukumo wa kuja kwenye biashara yako badala ya kwenda kwa wengine.
Tafakari;
Hakuna asiyependa vitu vizuri na kujaliwa. Kama biashara yako inatoa vitu vizuri na kuwajali sana wateja wake, wataendelea kuja kwenye biashara hiyo. Maana wanapata wanachotaka na kujaliwa pia.
Kocha.