2587; Kukamilika kila idara.

Kila aliyeoa au kuolewa, kuna vigezo alivyokuwa navyo vya aina gani ya mtu ambaye alitaka awe mke au mume wake.

Na kwa wengi vigezo hivyo vilitaka awe amekamilika kila idara. Yaani mwenye mlinganyo wa vitu vyote.
Sitakwenda kutaja vitu hivyo hapa, ila naamini picha umeipata.

Pamoja na vigezo hivyo, kila mtu aliyeoa au kuolewa hakuweza kupata mtu aliyekamilika kila idara.
Bali alipata mtu ambaye ana uimara kwenye baadhi ya vitu na udhaifu kwenye vitu vingine.

Wanaoweza kupokea uimara huo na kutojali sana udhaifu walionao wenza wao wanakuwa na maisha mazuri na ya maelewano.

Wanaolazimisha kuondoa udhaifu walionao wenza wao ili wakamilike kila idara kama wanavyotaka, wameishia kuwa na maisha ya hovyo na yasiyo na maelewano.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye safari ya mafanikio.
Wewe una uimara kwenye maeneo machache sana na udhaifu kwenye maeneo mengine mengi.

Ukichagua kuendeleza maeneo uliyo na uimara na kupuuza yale ambayo una udhaifu utaweza kufanya makubwa sana.
Lakini ukihangaika na kubadili madhaifu yako ili ukamilike kila idara, unaishia kuwa kawaida, maana madhaifu yako yanakuwa imara zaidi.

Muda ni mchache, nguvu zina ukomo. Unapotumia rasilimali hizo kwenye kitu kimoja, maana yake huwezi kuzitumia kwenye kitu kingine.

Changua vyenye wapi unawekeza rasilimali hizo, peleka kwenye kuimarisha uimara wako ili ufanye makubwa.
Usijisumbue kabisa na madhaifu yako.

Ukiwa vizuri kwenye uimara wako na kuweza kufanya makubwa, hakuna atakayejali sana kuhusu madhaifu yako.

Hatua ya kuchukua;
Ni madhaifu gani uliyonayo ambayo umekuwa unakazana kuyaboresha? Achana nayo na peleka nguvu zako zote kwenye uimara wako ili uweze kufanya makubwa.

Tafakari;
Unachokipa muda na nguvu zako ndiyo kinachokua zaidi. Ukiweka rasilimali hizo kwenye madhaifu yako ndiyo unayakuza zaidi. Ukiziweka kwenye uimara wako unaukuza zaidi. Chagua uwekezaji sahihi wa rasilimali zako muhimu.

Kocha.