#SheriaYaLeo (91/366); Sikiliza Sauti Yako Ya Ndani.

Ubobezi hautokani na uwezo ambao mtu amezaliwa nao au bahati.
Bali ni matokeo ya mtu kusikiliza sauti yake ya ndani na kufuata vile inavyomsukuma.

Kila mtu ana sauti hiyo ya ndani, ambayo inajua nini anataka kwenye maisha yake.
Ni sauti inayotokana na uwezo mkubwa na wa kipekee ambao mtu anao.
Lakini uwezo huo hauwezi kuonekana mpaka mtu aufanyie kazi.

Wengi hupuuza sauti zao za ndani na kufuata mkumbo wa kuishi kama wengine kwenye jamii.
Wanaishia kuwa walaji wa yale yanayozalishwa na wengine, huku wao wakiwa hawazalishi chochote.

Ni ubinafsi wa hali ya juu kama utaacha kuisililiza sauti yako ya ndani na kufuata mkumbo.
Unakuwa umeinyima dunia kitu cha kipekee kilicho ndani yako, ambacho kingekuwa na mchango mkubwa kwa wengine.

Maisha kuwa magumu, msongo, kukosa furaha na kuwa na chuki kwa wengine ni matokeo ya mtu kutokusikiliza sauti yake ya ndani na kufanya kilicho sahihi kwake.

Ukiwa na ushindi wa kutosha kwenye maisha yako, ambao unatokana na kuishi sauti yako ya ndani, huwezi kupata muda wa mambo mengine yasiyo na tija.
Huwezi kupata msongo au kuwachukia wengine, maana unakuwa umezama kweli kwenye kile kilicho sahihi kwako.

Uzuri ni kwamba sauti hiyo ya ndani huwa haipotei, hata ukiipuuza kwa muda mrefu kiasi gani, bado itaendelea kuwepo kwa kipindi chote cha uhai wako.
Hivyo muda wowote unaweza kuanza kuisikiliza sauti yako ya ndani na kuiishi.
Hakuna kuchelewa, wakati wowote ni sahihi kuiishi sauti yako ya ndani.

Sheria ya leo; Kwa kusikiliza na kuifuata sauti yako ya ndani, unagundua uwezo wako mkubwa na kuweza kuutumia kuonyesha upekee wako. Na hiyo ndiyo njia ya uhakika kwako kufikia ubobezi wa hali ya juu.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji