2593; Marudio.
Sijui ni mara ya ngapi narudia hili, lakini nimeshaliandikia hapa mara nyingi na narudia tena na tena na huu hautakuwa mwisho.
Marudio ndiyo mpango mzima.
Akili zetu huwa zinanasa vitu kutokana na kurudia rudia.
Kama wewe ni Mkristo na ukaamshwa usingizini kuambiwa usali sala ya Bwana, utafanya hivyo bila ya shaka.
Lakini zipo sala nyingine huwezi kufanya hivyo.
Tofauti siyo ugumu au urefu wa sala, bali marudio.
Angalia watoto, wanaweza kuimba na kucheza miziki maarufu kuliko wanavyoweza kukumbuka wanayofundishwa shuleni.
Yote hiyo ni kwa sababu ya marudio.
Kadiri unavyorudia rudia kitu kwa muda mrefu, ndivyo kitu hicho kinavyokaa ndani yako na kuwa sehemu yako.
Hupati ugumu wowote kwenye kula kila siku, kwa sababu umekuwa unakula kila siku.
Lakini unapata ugumu kwenye kusoma kila siku, japo ni kitendo kile kile cha kula, ila unalisha ubongo.
Sababu siyo huna muda au ni ngumu, sababu ni hujajenga utaratibu wa kufanya kila siku.
Hupati ugumu wowote kwenye kuongea kila siku, kwa sababu umekuwa unaongea kila siku.
Lakini unapata ugumu wa kuandika, kitu ambacho ni sawa na kuongea, ila kwa maandishi.
Siyo kwa sababu kuandika ni kugumu au kwa sababu huna cha kuandika, bali kwa sababu hujafanya uandishi kwa kurudia rudia mpaka ukawa sehemu yako.
Chochote unachotaka kufanya ili ufanikiwe, kuwa tayari kukirudia rudia bila ya kuchoka.
Kusoma, kuandika, kuongea na wateja, kufuatilia biashara na uwekezaji wako, yote hayo ni muhimu sana kwa mafanikio yako.
Hatua ya kuchukua;
Chagua vitu utakavyokuwa unafanya kwa kurudia rudia kila siku bila ya kuchoka kwa namna yoyote ile. Maana hivyo ndiyo vitakufikisha wewe kwenye mafanikio yako makubwa.
Tafakari;
Watu huwa wanakimbizana na vitu vipya kila wakati, lakini siri kuu ya mafanikio ipo kwenye kurudia rudia vile vya msingi kabisa.
Acha kukimbizana na mapya na weka marudio kwenye yale ya msingi.
Kocha.
Asante Sana kocha.
LikeLike