#SheriaYaLeo (97/366); Jifanye mjinga.
Kama lengo lako ni kufika ngazi za juu kabisa na kwa sasa uko ngazi za chini, kujionyesha kwamba ni mjuaji hakutakusaidia.
Zaidi kutakuwa kikwazo kwako, kwani wale walio juu watakuona wewe ni hatari kwao na kutumia kila njia kukuzuia usipande juu.
Lakini ukijifanya mjinga, walio juu wataona huna madhara yoyote na hivyo kukupa fursa kubwa na nzuri zaidi.
Wafanye watu waone wako juu zaidi yako kwenye kila eneo na hilo litawafanya wajisikie vizuri.
Kujisikia kwao vizuri kutakupa wewe fursa kubwa ya kufika kule unakotaka.
Hakuna wakati sheria hii ni muhimu kama zama hizi.
Wengi wamekuwa wanakimbilia kuanika mambo yao kwenye mitandao ya kijamii, wakitaka waonekane wako vizuri au wanapiga hatua kubwa.
Wasichojua ni wanakaribisha vikwazo mbalimbali, maana kadiri wengi wanavyojua mengi kuhusu wewe, ndivyo wanavyoyatumia kukukwamisha.
Mara zote wapotoshe watu kuhusu wewe, hasa wale ambao wanataka kukukwamisha usifike ngazi unazotaka kufika.
Wafanye waone wewe siyo hatari yoyote kwao na watakuacha ufanye yako.
Ila ukiwaonyesha kwamba wewe ni hatari kwao, watahakikisha wanakuondoa kabisa ili kujilinda wao wenyewe.
Sheria ya leo; Mara zote wafanye watu waamini wana akili na ni wajanja kuliko wewe. Hilo litawafanya wakuweke karibu na hilo litakupa wewe fursa za kupiga hatua kubwa zaidi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji