#SheriaYaLeo (109/366); Watoe maadui mafichoni.

Unaweza kuwa na maadui ambao wamejificha.
Ambao kwa nje wanaonekana kama marafiki, lakini kwa ndani wana uadui mkubwa.

Wanakuwa wanasubiri wapate fursa ili wakumalize.
Na kwa kuwa hujui, basi inakuwa rahisi kwako kuwapa fursa ya kutimiza lengo lao.

Katika safari ya mafanikio, adui usiyemjua ni hatari sana.
Kwani utamchukulia kama rafiki mwenye nia njema, kumbe mwenzako ana nia mbaya.

Uzuri ni kuna hisia na machale utayapata kwa mtu ambaye ni adui aliyejificha.
Kuna namna utakuwa na wasiwasi naye, lakini hutakuwa na udhibitisho, maana hajajiweka wazi.

Na hapo ndipo unahitaji kuchukua hatua ambayo itamtoa adui huyo mafichoni na kujidhihirisha wazi.

Fanya au sema kitu ambacho siyo sahihi, ambacho rafiki wa kweli hatakipa uzito sana.
Lakini adui aliyejificha atakipa uzito uliopitiliza.
Atanasa kwenye hisia kali ambazo haziendani kabisa na kile ulichofanya.

Na hapo utakuwa umethibitisha wazi kwamba kuna kitu kinaendelea ndani yake dhidi yako hivyo utapaswa kuwa na tahadhari kubwa kuhusu huyo.

SheriaYaLeo; Ukitaka kujua kama nyasi zina nyoka, unazipiga kwa fimbo. Ukitaka samaki wanase kwenye ndoano unawawekea chambo. Na ukitaka adui aliyejificha ajidhihirishe, fanya kosa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji