2608; Mategemeo yako kwa wengine.

Kila mmoja wetu huwa ana mategemeo fulani kwa watu wengine.

Lakini sehemu kubwa ya mategemeo hayo huwa siyo sahihi.

Kwa sababu hatujui kile kinachoendelea ndani ya mtu.

Unaweza kuwa unategemea mtu awe kwa namna fulani yeye akawa kwa namna ya tofauti.

Ukadhani labda amefanya kwa makusudi, kumbe kuna mambo anayopitia yanayopelekea awe hivyo.

Hivyo pamoja na kuwa na mategemeo fulani kwa wengine, usikimbilie kuhukimu pale wanapokwenda tofauti na mategemeo hayo.

Kama hujajua kinachoendelea ndani ya mtu, basi epuka sana kukimbilia kuhukumu, kwani haina msaada kwako wala kwa wengine.

Na muhimu zaidi, usimhukumu mtu kwa kitu kimoja.
Usisahau mazuri yote ambayo mtu amewahi kufanya kwa sababu ya kitu kimoja alichofanya tofauti na ulivyotegemea.

Wape watu nafasi, kuna mengi yanaendelea kwenye maisha yao ambayo huwezi kuyajua.

Hatua ya kuchukua;
Pale mtu anapofanya tofauti na ulivyotegemea afanye, usikimbilie kumhukumu na kuona hafai.
Badala yake taka kujua kwa undani zaidi au mpe nafasi zaidi, huwezi kujua nini anapitia.

Tafakari;
Unawachukulia watu vile unavyotaka wewe na siyo walivyo wao.
Hivyo wanapokwenda tofauti na unavyotaka, usikimbilie kuona hawafai, huenda hawapo sawa.

Kocha.